Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Kalambo Francis Mapunda kulia na Diwani wa kata ya Kisumba Innocent Lungwa kushoto wakimsikiliza mhandisi wa maji kutoka ofisi ya meneja wa Ruwasa wilaya ya Kalambo Marwa Webiro kuhusu maendelea ya ujenzi na upanuzi wa mradi wa maji Kisumba.
Baadhi ya mabomba yatakayotumika kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji Kisumba kata ya Kisumba wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.
Tenki la kuhifadhi lita 200,000 za maji linalojengwa katika mradi wa maji Kisumba wilayani Kalambo ukiendelea.
Na Muhidin Amri,
Kalambo
WAKALA wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)inatarajia kutumia Sh.bilioni 1.8 kwa ajili ya kufanya upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji Kisumba kata ya Kisumba Halmashauri ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Kalambo Francis Mapunda alisema,mradi huo utahudumia zaidi ya wakazi 12,000 wa vijiji vinne vya Kafukoka,Kisumba,Kasote na Kisenga.
Mapunda alitaja kazi zinazotekelezwa katika upanuzi wa mradi huo ni ujenzi wa tenki la lita laki mbili kwa ajili ya kuhudumia wakazi wa vijiji vitatu na tenki moja la lita 50,000 litahudumia wakazi 4,000 wa kijiji cha Kafukoka.
Aidha alisema,Ruwasa imekamilisha mradi wa maji katika kijiji cha Kalaela kwa gharama ya Sh.milioni 436 zilizotolewa na serikali kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uvico-19 ambao unahudumia wakazi 3,500 wa kijiji hicho.
Alisema,katika mradi huo wamejenga vituo vya kuchotea maji katika maeneo mbalimbali na tayari watu zaidi ya 20 wameomba kuingiziwa huduma ya maji majumbani.
Mapunda alisema,watu wasiokuwa na uwezo huo wataendeleo kuchota maji kupitia vituo maalum vilivyojengwa(DPS) na kuwataka wananchi kuhakikisha wanatunza miradi ya maji iliyojengwa katika maeneo yao ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Diwani wa kata ya Kisumba Innocent Lungwa,ameiomba serikali kupitia Ruwasa kukamilisha upanuzi wa mradi wa maji Kisumba ili kuwaondolea kero wananchi wa kata hiyo kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.
Alisema,kero ya maji katika kata hiyo ni kubwa hasa katika vijiji vinne vya Kafukoka,Kisenga,Kasote na Kisumba,hata hivyo ameishukuru serikali kutoa fedha za upanuzi wa mradi huo.
Alisema,mradi wa zamani uliojengwa tangu miaka ya themanini hautoshelezi mahitaji ya watu waliopo,hivyo upanuzi wa mradi huo utasaidia kwa kiwango kikubwa kumaliza kero ya maji safi na salama.
Msimamizi wa ujenzi wa mradi huo Aziz Ismail alisema,kazi ya ujenzi wa mradi huo ulianza mwezi 4 na unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka.
Alisema,kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa tenki la maji la ujazo wa lita 200,000 ujenzi wa chanzo cha maji,vituo vya kuchotea maji,uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba.