Na John Walter-Babati
Hatimaye michuano ya Chemchem iliyodumu kwa kipindi cha mwezi mmoja imehitimishwa kwa Mac Lion FC kuchukua ubingwa kwa mwaka 2023.
Mac Lion wamepata ubingwa huo baada ya kuichapa mabao 2-0 Macedonia FC.
Akifunga Michuano hiyo Afisa Michezo, Utamaduni na Sanaa mkoa wa Manyara Samwel Pastori, ameipongeza taasisi ya Chemchem Association kwa kuwa wabunifu katika kufikisha elimu kwa jamii juu ya uhifadhi kupitia michezo.
Amesema nichezo hiyo licha ya kuibua vipaji kwa vijana na kuimarisha afya zao lakini pia inawafanya watumie muda mwingi kufanya mazoezi na kuepuka vitendo visivyofaa katika jamii ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha amewapongeza waandaaji wa ligi hiyo kwa kuwa na uwanja mzuri wenye majukwaa usiopatikana katika kijiji chochote katika mkoa wa Manyara na kuwataka kuangalia namna nzuri ya kuuboresha zaidi.
Mashindano hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Mdori kata ya Nkaiti wilaya ya Babati mkoani Manyara yametumia Shilingi Milioni 99.
Lengo la Mashindano hayo ni kupiga vita ujangili wa wanyama pori pamoja na kuibua vipaji vya soka kwa vijana ambapo kwa mwaka huu yalioongozwa na Kauli mbiu isemayo OKOA TWIGA.
Timu zote 31 zilizoshinda za wanawake, vijana wenye umri chini ya miaka 18 na za wakubwa zimekabidhiwa zawadi mbalimbali zikiwemo fedha na mipira huku timu zilizofanya vizuri na wachezaji bora nao wakizawadiwa.
Mkurugenzi wa ChemChem Association, Nicolas Negre amesema michuano hiyo tangu imeanzishwa imekuwa na faida kwani imewaleta wananchi karibu ambao wengi wamepokea ujumbe wa mwaka huu wa kulinda Twiga.
Mashindano hayo yamedhaminiwa kwa asilimia mia moja na taasisi ya Chemchem inayofanya shughuli za Utalii na Uhifadhi katika eneo la Hifadhi ya jamii ya wanyamapori Burunge inayozungukwa na vijiji kumi.