Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe.Harusi Said Suleiman akizungumza machache wakati akizindua Bodi ya Maamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) huko Ofisi za Mazingira Maruhubi Mjini Unguja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe.Harusi Said Suleiman akimkabidhi kabrasha lenye nyenzo za kufanyia kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Maamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) Asha Ali Khatib mara baada ya kuizundua bodi hiyo huko Ofisi za Mazingira Maruhubi Mjini Unguja.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR.
Na Fauzia Mussa-Maelezo
Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu,weledi, umakini na kujituma ili kuirudisha Zanzibar katika hali yake nzuri ya kimazingira.
Akitoa nasaha kwa wajumbe hao wakati akizinduzi Bodi hiyo huko Ofisi ya ZEMA Maruhubi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe.Harusi Said Suleiman amesema kufanya hivyo kutapelekea dhamira ya kuteuliwa kwao kufanikiwa kwa ufanisi mkubwa.
Alisema kwa sasa Zanzibar inakabiliwa na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi kulikosababishwa na uchimbaji wa mchanga sehemu zisizo rasmi pamoja na ukataji wa miti ovyo hivyo bodi hiyo ina kazi kubwa ya kutatua changamoto za athari hizo amabazo zimejitokeza nchini.
Alisema uwepo wa mazingira rafiki kwa viumbe wa misitu na bahari kunaleta ustawi wa maendeleo ya nchi hivyo aliwataka wajumbe wa bodi hiyo kuzingatia miongozo, kanuni na sheria za kusimamia mazingira ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia nchi juu ya viumbe hao.
Waziri Harusi aliwasisitiza wajumbe hao kubuni mikakati ya kidigitali na vyanzo vya mapato ili kuiwezesha Taasisi hiyo kujitegemea na kuwataka watendaji hao kuwa na mashirikiano mazuri na Wananchi ili kugundua kwa haraka athari za kimazingira na kuzipatia ufumbuzi.
Nae Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa mazingira ZEMA Asha Ali Khatib amesema bodi hiyo itahakikisha kuwa inatekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuimarisha ustawi wa mazingira Nchini.
Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira imeteuliwa hivi karibuni kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2015 ikiwa na jukumu la kusimamia uhifadhi wa mazingira nNchini