Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera akiwa katika kikao cha majadiliano ya uwekezaji na wawakilishi wa kampuni ya Planet Smart City leo Jijini Dodoma.
Kikao cha Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera akiwa katika kikao cha majadiliano ya uwekezaji na wawakilishi wa kampuni ya Planet Smart City kilichofanyika leo Jijini Dodoma.
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera akisilikiliza katika kikao cha majadiliano ya uwekezaji na wawakilishi wa kampuni ya Planet Smart City mapema leo Jijini Dodoma.
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera (katikati) baada kikao cha majadiliano ya uwekezaji na wawakilishi wa kampuni ya Planet Smart City kilichofanyika leo Jijini Dodoma.
Na mwandishi wetu Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekutana na wawakilishi wa kampuni ya Planet Smart City ya Uingereza ili kujadiliana kuhusu mpango wa uwekezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu hapa nchini.
Kupitia mjadiliano na wawekezaji hao Naibu Katibu Mkuu Lucy Kabyemera amesema wamepokea mapendekezo ya mpango mkakati wa kampuni hiyo kwa ajili ya kuupitia huku akiweka bayana upo uwezekano wa kufanya nao kazi kutokana na uhitaji mkubwa wa nyumba nchini.
Bi. Kabyemera alibainisha hayo mapema leo Jijini Dodoma alipowakaribisha wawekezaji hao ofisini kwake na kubainisha kuwa uwekezaji huo unakuja kufuatia matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ambayo imesukuma kampuni hiyo kuja hapa Nchini.
‘’Sensa ya watu na makazi imeonesha kuwa kuna upungufu wa zaidi ya nyumba Mil.3 na mahitaji ya nyumba hapa Nchini ni takribani 390,000/= kila mwaka hivyo fursa hii ya ujenzi wa nyumba ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan’’ Alisema Bi. Lucy Kabyemera Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi.
Pia, Naibu katibu Mkuu amesema wizara inaangalia njia sahihi na bora ya kuweza kufanya kazi na kampuni hii hasa ukilinganisha uwezo wa kifedha wa wananchi pamoja na gharama za vifaa vya ujenzi hivyo kuona uwezekano wa kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifesha ikiwemo mabenki ya hapahapa nchini.
Bi. Kabyemera amebainisha pia kuwepo kwa faida lukuki kwa wazawa kupitia mradi huo kwani utekelezaji wake utahusisha kutumia wataalamu wazawa na vijana kama nguvukazi ya utekelezaji wa mradi huo.
‘’Endapo tutafanikiwa kufikia makubaliano na kampuni hii yapo manufaa mengi ikiwa ni fursa ya vijana wetu kujipatia ajira lakini na sio hao tu hata mama ntilie na wazalishaji wa vifaa vya ujenzi wataweza kunifaika pia ’’. Alisema Bi. Lucy Kabyemera Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Upendo Matotola amesema kuwa utekelezaji wa mradi utahusisha ujio wa teknolojia ya kisasa katika sekta ya ujenzi ikiwemo miundo mbinu ya barabara jambo ambalo litakuwa na manufaa makubwa kwa watanzania.
‘’Kwa Wizara tunaona ni kitu kizuri wao kuja kwa hiyo tumewasikiliza na wao kuna baadhi ya taarifa wanazihitaji ili kuhakikisha wanapata taarifa sahihi ili wanapokuja wanakuja kuwekeza wanakuwa wana taarifa sahihi. ”Aliongeza Dkt. Matotola.
Dkt. Matotola ametoa wito kwa watanzania endapo utekelezaji wa mradi huu utafanikiwa basi wawe tayari kuupokea kwani ujenzi wa makazi ya pamoja hupunguza gharama kubwa licha ya ukweli kwamba bado watu wengi hawana utamaduni wa makazi ya pamoja.
Kampuni ya Planet Smart City ni ya uingereza ambayo kabla ya kuja Tanzania tayari imekwisha anzisha miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba katika mataifa ya Brazil na India naimevuiwa kuvutia mataifa mengi duniani ikiwemo Tanzania.