Baadhi ya majengo ya kutolea huduma za afya yaliyojengwa katika Hospitali ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa Shafi Mpenda,akizungumza na baadhi ya wananchi waliofika katika Hospitali ya wilaya Kalambo ili kupata huduma za matibabu.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Matai wilayani Kalambo wakisubiri kupata matibabu katika Hospitali ya wilaya Kalambo.
Muuguzi kiongozi wa Hospitali ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa Didi,akimwelekeza namna ya kunyonyesha mtoto mkazi wa kijiji cha Matai Hellen Kashije baada ya kujifungua.
Na Muhidin Amri,
Kalambo
HALMASHAURI ya wilaya Kalambo Mkoani Rukwa,imepokea jumla ya Sh.bilioni 3,440,000,000 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kujenga Hospitali ya wilaya ili kuimarisha na kusogeza huduma za afya kwa wananchi.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Shafi Mpenda,wakati akizungumza na wananchi waliokutwa wakisubiri kupata huduma za matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Kalambo.
Alisema,katika awamu ya kwanza mwaka 2018/2019,Halmashauri ilipokea Sh.bilioni 1.5 kutoka serikalini kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala, jengo la wagonjwa wa nje(OPD),maabara,jengo la dawa,jengo la kufulia nguo na jengo la huduma za mionzi(X-ray) ambayo ujenzi wake umekamilika na yanatoa huduma.
Mpenda alisema, kwa mwaka wa fedha 2019/2020,wamepokea Sh.milioni 300 kwa ajili ya umaliziaji wa majengo saba ili kuiwezesha Hospitali kuanza kutoa huduma kwa jamii ujenzi wa baadhi ya majengo,hata hivyo hayakuweza kukamilika kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mpenda,mwaka 2020/2021 serikali ilitoa Sh.milioni 500 ili kujenga wodi tatu ikiwemo ya wanawake,wanaume na watoto na katika awamu ya nne ya mwaka wa fedha 2022/2023 wamepokea Sh.bilioni 1,140,000,000.00.
Mpenda alifafanua kuwa,kati ya hizo Sh.milioni 800 zimetumika kujenga wodi ya upasuaji kwa wanawake na wanaume,jengo la kuhidhia maiti na jengo la upasuaji na Sh.milioni 250 zimetumika kujenga wodi ya wagonjwa mahututi.
Aliongeza kuwa, Sh.milioni 90 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi watatu(3 in 1) ili waweze kuishi karibu na Hospitali na kutoa huduma kwa haraka pindi wanapohitajika.
Pia alisema, Halmashauri kupitia mapato ya ndani imefanikiwa kujenga jengo la mama na mtoto ambalo limekamilika na wananchi hasa akina mama wameanza kupata huduma.
Katika hatua nyingine Mpenda,amewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa na watumishi kwenye taasisi za umma ili iweze kufanya maboresho na kuchukua hatua.
Mpenda alisema,hatua hiyo itaisaidia sana serikali kutambua na kubaini mapungufu ya watumishi wake na huduma inazotoa kwa wananchi wanapofika kwenye taasisi zake zikiwemo zinazotoa huduma za afya.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya Kalambo Kisyombe alisema,katika Hospitali hiyo kuna jumla ya majengo 15 yaliyoanza kutoa huduma za afya kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Dkt Kisyombe,alitaja huduma zinazotolewa ni za wagonjwa wa nje,huduma za kulaza na kwa siku wanahudumia kati ya wagonjwa 30 hadi 40 na kwa mama wanaofika kwa ajili ya huduma za kliniki na uzazi wa mpango ni 20 hadi 30.
Alisema kuanzia mwezi Februari hadi Oktoba 2023,Hospitali hiyo imehudumia zaidi ya wananchi 800 wenye matatizo mbalimbali ya kiafya wakiwemo akina mama waliofika kwa ajili ya kujifungua ambapo kati ya wajawazito 60 wajawazito 5 walijifungua kwa njia ya upasuaji.
Mkazi wa kijiji cha Matai yalipo makao makuu ya wilaya ya Kalambo Marietha Masole,ameishukuru serikali kujenga Hospitali hiyo kwa kuwa imewasogezea huduma za afya karibu na maeneo yao.
Hata hivyo,ameshauri kuongezwa watumishi ili wagonjwa wanaofika waweze kupata matibabu haraka badala ya kukaa muda mrefu kusubiri jambo linalosababisha kupoteza muda mwingi kusubiri kupata huduma.