NJOMBE
Wakala wa usajili biashara na Leseni Brela imetumia maonesho ya viwanda vidogo na Kati ya SIDO awamu ya nne yanayofanyika mkoani Njombe katika viwanja vya sabasaba kutoa elimu kwa wananchi hususani wafanyabiashara na wajasiriamali juu ya umuhimu wa huduma zao katika sekta ya biashara na uwekezaji.
Akizungumza katika maonesho hayo,msaidizi wa usajili mwandamizi kurugenzi ya miliki ubunifu kutoka wakala wa usajili wa biashara na leseni BRELA Nassoro Mtavu,amesema taasisi hutumia matukio yanayokutanisha watu wengi yakiwemo maonyesho ili kutoa elimu kwa wananchi ya usajili wa majina ya biashara ,usajili wa makampuni ,Leseni za biashara na viwanda ,alama za bidhaa na huduma na nyingine nyingi huku Lengo likiwa kuwapunguzia changamoto ya kufata mbali huduma zao.
Aidha Brela imewataka wamiliki wa biashara na makampuni wenye uhitaji na huduma baada ya usajili Kama vile kubadili anwani za ofisi na binafsi pamoja huduma ya kubadili majina ya watu katika makampuni ili kuendana mahitaji ya wakati huo.
“Lakini kitu ambacho tumekiona kwenye maonesho haya na tunajaribu kuona namna nzuri ya kufikisha ujumbe ni wateja wetu wamekua wakichanganya majina ya biashara na alama za biashara sasa ni kitu ambacho tunaendelea kutoa elimu kwa taratibu kwa sehemu kubwa wanaelewa na wanaitika”alisema Mtavu.
Awali akizindua maonyesho hayo naibu waziri wa viwanda na biashara Exaud Kigahe amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ili kuongeza ustawi wa viwanda na biashara na Kisha kufungua mipaka ili kuuza bidhaa za mazao nje ya nchi kwa sababu bado kuna watanzania hawajatumia vema soko la Jumuia ya Afrika Mashariki.
“Niwahakikishie kuwa iwapo tutaunganisha kilimo na viwanda tutaweza kukuza soko la ndani lakini pia kupunguza uagizaji bidhaa ambazo tunaweza kuzizalisha sisi wenyewe kutokana na mazao ya kilimo na malighafi nyingine ambazo tunaweza kuzalisha ndani,lakini zaidi tutaweza kuingiza bidhaa zetu katika masoko ya nje na ya kimataifa”anasema Kigahe.
Kigahe amesema serikali imejipanga kuhakikisha inalisha dunia na afrika kwa bidhaa ambazo zimeongezwa thamani.”Sio kuuza nje parachichi kama ilivyo,kuuza mahindi kama yalivyo,alizeti na mengineyo,tuuze unga,tuuze bidhaa zilizoongezwa thamani.
Aidha amelitaka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo SIDO kushirikiana na Halmashauri ili kuhakikisha vijana wanapata teknolojia ili kuweza kifanya kilimo kibiashara.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka,mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amemshukuru Rais Samia kwa kutoa ruzuku kwenye mbolea ili kuongeza uzalishaji kwenye mazao ya chakula.