Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua katika shule za msingi mkoani Singida uliofanyika Oktoba 24, 2023 mkoani Singida. Wengine kutoka kushoto ni Meneja MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Lodovick na Mwakilishi wa Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya , Theresia Shirima. Vyandarua hivyo vitasambazwa na MSD katika shule hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki uzinduzi huo.
Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Gari la MSD likiwa na shehena ya vyandarua hivyo tayari kwa usambaji.
Na Dotto Mwaibale, Singida
BOHARI ya Dawa (MSD) imeanza kusambaza vyandarua zaidi ya 341,000 vyenye dawa katika shule za msingi mkoani Singida kwa lengo la kutokomeza ugonjwa wa malaria ifikapo 2030.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua katika shule za msingi mkoani Singida, Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa alisema kazi hiyo ya usambaji wa vyandarua hivyo itafanyika kwa wiki tatu.
Alisema MSD ndio yenye mamlaka ya kisheria ya Kununua, Kuzalisha, Kuhifadhi na Kusambaza bidhaa za Afya hapa nchini ndio maana wanafanya kazi hiyo.
Alisema MSD wanasambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara na kuwa vyandarua vinaingia kama vifaa tiba ambavyo vinatumika kumkingia mwananchi asishambuliwe na malaria.
“MSD leo tupo mkoani Singida kushuhudia uzinduzi wa usamabazi wa vyandarua zaidi ya 341,000 kwenye shule za msingi katika halmashauri za wilaya sita isipokuwa moja ya Singida Manispaa na hilo ndilo jukumu tulilopewa na zoezi hili la ugawaji wa vyandarua hivi tunatarajia kulifanya kwa kipindi cha wiki tatu,” alisema Jumaa.
Alisema ili zoezi hilo liweze kukamilika wanahitaji kupata ushirikiano kwa wadau wote ambao ni sehemu ya usambazi huo ambao ni wakuu wa wilaya, wakurugenzi, maafisa elimu kuanzia mkoani hadi kwenye kata na wakuu wa shule na kwa ushirikiano huo unaweza kuwafikisha kwenye lengo walilojiwekea.
Alisema MSD imepewa jukumu hilo kutokana na uzoefu mkubwa walionao na kuwa na miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ya kielektroniki kuanzia kuhifadhi hadi usambazaji.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi akizindua kampeni hiyo alisema ugonjwa wa malaria bado ni tatizo mkoani hapa kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2022 ulioonesha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria kipo wastani wa asilimia 1.5 ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimia 8.4 (TMIS 2022)
Alisema Halmashauri ya Itigi inakiwango kikubwa zaidi ya maambukizi ya asilimia 9.8 ukilinganisha na Halmashauri ya Singida ambayo ina kiwango cha chini zaidi ya asilimia 0.0 na kueleza kuwa Serikali bado inaendelea na juhudi za kuhakikisha inatokomeza kabisa ugonjwa hatarai wa malaria kufikia 2030.
Mwakilishi wa Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya , Theresia Shirima alisema adhima ya Serikali ni kuhakikisha hadi ifikapo 2030 ugonjwa wa malaria unatokomezwa kabisa kwa kufanya usafi, kuharibu mazalia ya mbu na njia nyingine ikiwamo ya ugawaji wa vyandarua mashuleni ambapo wanafunzi watasaidia kuvifikisha kwenye kaya wanazotoka.
Alisema walengwa zaidi katika hizo kaya ni yale makundi ambayo yanakuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo ambao ni wajawazito na watoto walio chini ya miaka mitano.
Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Dkt. Elpidius Baganda alisema vyandarua hivyo vinakwenda kugaiwa katika shule 670 na alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo ambayo ni muhimu kwa taifa.