Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa Shafi Mpenda kushoto,akimsikiliza Mkuu wa shule ya Sekondari Chilengwe kata ya Mnamba Vicent Nandi kuhusu maendeleo ya ujenzi wa nyumba ya Mwalimu ambayo ujenzi wake haujakamilika hadi sasa,wa pili kushoto Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Erasto Mwasanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa Shafi Mpenda kushoto na Afisa mipango wa Halmashauri hiyo Erasto Mwasanga wa pili kushoto,wakimsikiliza fundi aliyepewa kazi ya kujenga nyumba ya kuishi Mkuu wa shule ya Sekondari Chilengwe Gerald Kazonda kulia,kuhusu kuchelewesha ujenzi wa nyumba hiyo.
Baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule mpya ya Sekondari ya Chilengwe kata ya Mnamba wilayani Kalambo.
Wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Chilengwe Halmashauri ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa wakiwa darasani.
…
Na Muhidin Amri
Kalambo
SERIKALI imetoa Sh.milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari katika kata ya Mnamba Halmashauri ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa,ili kuwaondolea adha wanafunzi wanaotoka katika kata hiyo kwenda nchi jirani ya Zambia kufuata elimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kalambo Shafi Mpenda alisema,kata hiyo haikuwa na shule ya sekondari hivyo wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga na sekondari walilazimika kwenda shule ya Mambwe iliyopo umbali wa kilomita 17.5 na nchi jirani ya Zambia kuendelea na masomo yao.
Alisema,serikali imefanya jambo jema kujenga shule hiyo kwani itawawezesha watoto wanaotoka katika kata ya Mnamba kusoma shule ya jirani hivyo kuwaondolea usumbufu wa muda mrefu ambao uliosababisha baadhi ya watoto kukatisha masomo kutokana na changamoto hiyo.
Alisema,shule hiyo imesajiliwa na imeshaanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2023 na watoto wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza(Pre- Form One) kwa mwaka wa masomo 2024.
Alisema,uwepo wa shule hiyo ni faraja siyo kwa wanafunzi tu bali hata kwa wazazi kwa kuwa hawalazimiki kuingia gharama ya usafiri kwa ajili ya watoto wao kwani sasa shule ipo jirani na maeneo yao na kuishukuru Serikali kwa kutoa fedha zilizofanikisha ujenzi wa shule hiyo.
Katika hatua nyingine Mpenda alisema,Halmashauri ya wilaya Kalambo imepokea kiasi cha Sh.milioni 100 kwa ajili ya kujenga nyumba ya kisasa ya Mkuu wa shule.
Alisema,nyumba hiyo itakapokamilika itamwezesha mwalimu atakayeishi katika nyumba hiyo kutekeleza majukumu yake kwa utulivu mkubwa na kumuondolea adha ya kupanga nyumba kwa wenyeji.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Vicent Nandi alisema,shule imeanza rasmi mwaka wa masomo 2023 na ilipangiwa kuchukua wanafunzi 200 wa kidato cha kwanza lakini kutokana na changamoto mbalimbali wanafunzi waliopo shuleni ni 167 wanaoendelea na masomo.
Alisema,awali mazingira ya elimu katika kata ya Mnamba hayakuwa mazuri kwani watoto wanaochaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari walilazimika kwenda nchi jirani ya Zambia na wengine kata za jirani kufuata masomo yao.
Nandi,ameiomba serikali kuendelea kuwasaidia kwa kujenga mabweni ili watoto wote waweze kuishi kwenye mazingira ya utulivu, kwani baadhi yao wanatoka katika mazingira magumu na wengine kupanga vyumba uraiani jambo ambalo ni hatari hasa kwa wanafunzi wa kike.
Wanafunzi wa shule hiyo wameishukuru serikali kuwajengea shule ambayo imemaliza usumbufu na kero ya muda mrefu kwenda nchi jirani ya Zambia kufuata masomo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake Efrem Adam alisema,shule hiyo ni mahitaji yao ya muda mrefu kwani kila mwaka wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari walilalazimika kuvuka mpaka na kwenda kusoma nchini humo.
Alisema,hali hiyo imesababisha baadhi ya wanafunzi kukatisha masomo kutokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata masomo na kuepuka gharama za usafiri zinazotakiwa kulipwa na wazazi wao.