Picha ya pamoja ya baadhi ya washiriki baada ya mafunzo hayo
Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame akifunga mafunzo hayo
Meneja wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Cheick Sangare akimkaribisha Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame wakati wa mafunzo hayo.
Mhandisi Migodi kutoka Tume ya Madini, Mackenzie Mabula,akitoa mada
Washiriki wakifuatilia mada mbalimbali
Washiriki wakifuatilia mada mbalimbali
Picha ya pamoja ya Meneja wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare pamoja na baadhi ya viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama wa Nyang’hwale na Msalala
*
Katika kuboresha utekelezaji wa Miradi itokanayo na uwajibikaji wa jamii (CSR) Mgodi wa Barick Bulyanhulu kwa kushirikiana na Tume ya Madini wameendesha mafunzo kwa watumishi wa Halmashauri wilaya za Nyang’hwale kutoka mkoani Geita na Msalala mkoani Shinyanga juu ya Kanuni za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii CSR za mwaka 2023.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika katika Mgodi wa Bulyanhulu, mwishoni mwa wiki yalifungwa na Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, ambaye ameupongeza mgodi huo kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia watalamu kutoka halmashauri ya wilaya hizo 2 kutekeleza kwa ufanisi Miradi ya Kijamii inayotekelezwa kwa fedha kutoka Barrick Bulyanhulu.
“Tunaipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuwezesha upatikanaji wa kanuni hizi, na nina imani kupitia mafunzo haya miradi yote itasimamiwa vizuri zaidi katika kipindi cha mwaka ujao ili kufanikisha lengo lililokusudiwa na kunufaisha wananchi”,amesema
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Khamis Katimba, ameishukuru Barrick Bulyanhulu kwa kuandaa mafunzo hayo ambapo amesema Halmashauri yake inanufaika kwa kiasi kikubwa na uwekezaji uliofanywa na Mgodi huo kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imetekelezwa katika halmashauri hiyo.
Bw.Katimba, alisema ni muhimu miradi ya CSR kuzingatia kubadilisha maisha ya wananchi walio maeneo yaliyo na uchimbaji wa madini na kuhimiza uaminifu na uadilifu kwa maofisa wanaosimamia miradi hiyo ili kuleta tija kwa wananchi huku akiainisha changamoto ambazo zilikuwa zinatokana na kutokuwa na kanuni kama vile miradi kutotekelezwa kwa wakati, kupishana kwa mtazamo kati ya halmashauri na migodi pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya CSR.
Akiwasilisha kanuni hizo Mhandisi Migodi kutoka Tume ya Madini Makao Makuu Mackenzie Mabula, alisema kuwa kanuni hizo mpya zitatumika kwa wamiliki wa leseni za madini ambapo zinatarajiwa kuwasaidia sana waatalamu na wasimamizi wa miradi ambayo itatekelezwa kupitia CSR.
Aidha amezitaka Halmashauri hizo kuzifuata kanuni hizo ili kurahisisha uandaaji na utekelezaji wa Miradi.
“ Niwaombe sana kanuni hizi ni rafiki sana katika utekelezaji wetu hivyo tuzifuate inavyotakiwa kwani awali tulikuwa na sheria pekee jambo ambalo lilikuwa linawapa ugumu kuzichambua sheria zote sasa tutumie kanuni hizi kutekeleza Miradi yetu”, alisema Mabula.
Kwa Upande wake Meneja wa Mazingira na Mahusiano ya jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Agapiti Paul, ameziomba Halmashauri hizo kuendelea kushirikiana na mgodi ili kufanikiwa kukamilisha miradi kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji uliofanywa na Mgodi huo.