Wahitimu wa kidato cha sita katika shule ya mchepuo wa kiingireza ya St Mary’s Duluti iliyopo Tengeru mkoani Arusha wakiburudisha katika mahafali hayo mkoani Arusha .
Julieth Laizer,Arusha .
Arusha .Wahitimu wa kidato cha sita nchini wametakiwa kusoma kwa malengo na kutumia vipaji walivyo navyo na kuviendeleza kwa manufaa ya maisha yao ya baadaye.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mwenyekiti wa wakuu wa shule za sekondari Tahosa Arusha Dc,Joseph Sunday Maliya wakati akizungumza katika mahafali ya 10 ya shule ya mchepuo wa kiingireza ya St. Mary’s Duluti iliyopo Tengeru mkoani Arusha .
Aidha amewataka wahitimu hao kufanya kazi kwa bidii na wahakikishe wanasoma kwa bidii wasikariri masomo ya darasani tu huku wakihakikisha wanaepukana na vitendo viovu ikiwemo maswala ya ushoga na mambo mengine.
Hata hivyo amewataka kuwa mstari wa mbele kukemea matendo maovu huku akiwaonya wanafunzi hao kuepukana na kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa ambayo mwisho wa siku yanawaharibia malengo yao .
“Hapa mlipohitimu bado sana ndo kwanza mmeanza safari ya kujiendeleza naombeni mhakikishe mnajituma ili muweze kufikia malengo yenu na mkawe mfano bora wa kuigwa katika jamii.”amesema.
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari ya St .Mary’s Duluti ,Br. Essau Mlengule amesema kuwa shule hiyo imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha elimu inazidi kupanda siku hadi siku kutokana na mikakati mbalimbali waliyojiwekea .
Aidha amesema kuwa, shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007 na imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma kufuatia wanafunzi wengi kufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu.
Amefafanua kuwa ,while imekuwa na mikakati mingi ikiwemo kuondoa daraja la tatu ikiwezekana kuongeza daraja la kwanza .
“Changamoto kubwa iliyopo ni mwamko mdogo wa baadhi ya wanafunzi kutopenda kujisomea makala mbalimbali ambapo ametoa wito kwa wanafunzi hao kupenda kujisomea makala kwani ndio kisima cha maarifa “amesema .
Aidha amewataka wahitimu kujitahidi kujifunza na kuwa makini kwani bado safari ni ndefu sana bila kuweka malengo yao hawataweza kutatua changamoto katika jamii inayowazunguka.
Hata hivyo amewataka wanafunzi hao kutambua kuwa elimu waliyoipata ikafanyike msaada katika jamii inayowazunguka kiroho na kiuchumi na wakubali kubadilika katika mienendo yao kwani wao ndio kioo cha kuigwa kwenye jamii.
Nao wahitimu wa kidato cha sita wakizungumza katika mahafali hayo wameshukuru uongozi wa shule hiyo kwa namna ambavyo wamewaandaa vizuri na kuwajengea kujiamini sambamba na kuweza kujitegemea wao wenyewe.