Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe Mhe. Fatuma Toufiq (kushoto) akieleza jambo wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bungeni , Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bungeni, Jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (kushoto) akichangia jambo wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Hufadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Bungeni, Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mbarouk Magawa akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Bungeni Jijini Dodoma
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Dkt. Aggrey Mlimuka akizungumza wakati wa kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Bungeni Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa Idara, Vitengo na Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu pamoja na Watendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wakifuatilia maelezo ya wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mfuko huo, Bungeni, Jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, imeridhishwa na dhamira ya serikali ya kuimarisha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ikiwamo kulipa Sh.Trilioni 2.17 ambazo ni sehemu ya deni la michango ya watumishi wa kabla ya Mwaka 1999.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe.Fatuma Toufiq ameyasema hayo katika kikao cha kamati hiyo cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya PSSSF uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Amesema kamati inampongeza Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mfuko huo ambapo Desemba 15, 2021 serikali ilitoa fedha hizo na kulipa madeni ya uwekezaji sh.Bilioni 500 kati ya Sh.bilioni 731 zilizohakikiwa.
Mhe. Toufiq amehimiza mfuko kutoa elimu ya kujiandaa kustaafu kuanzia kwa waajiriwa wapya ili wafanye maendeleo na kujiwekea akiba mapema badala ya kusubiri hadi wastaafu.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Prof.Joyce Ndalichako, amesema serikali itaendelea kuimarisha uhai wa mfuko huo na kuahidi kufanyia kazi ushauri uliotolewa na kamati hiyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe.Patrobas Katambi, amesema serikali imetengeneza mifumo ya kisheria inayolenga kuleta ustawi kwa watumishi wanapostaafu.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba, amesema hatua zingine zilizochukuliwa na serikali kuboresha mfuko huo ni pamoja na kuzuia uwekezaji kwenye maeneo yasiyo na tija na kuweka ukomo wa uwekezaji ili kuleta ufanisi.