Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, (FAO), Dkt. Qu Dongyu baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika kwenye makao makuu ya shirika hilo , Rome nchini Italia Oktoba 18, 2023. Mheshimiwa Majaliwa anamuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani linalofanyika makao makuu ya FAO kuanzia Oktoba 16, 2023 hadi Oktoba 20, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Ni kuhusu utekelezaji mradi wa BBT, aahidi kuitembelea 2024
*Waziri Mkuu asema Serikali imetenga bil. 900 kuimarisha umwagiliaji
MKURUGENZI MKUU wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) Dkt. Qu Dongyu amesema kuwa Shirika hilo limevutiwa na mradi wa kuwawezesha vijana unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania wa Jenga Kesho Iliyobora “Building Better Tomorrow” (BBT).
“FAO tutaunga mkono mradi huu ili Serikali ya Tanzania iweze kutimiza malengo ya kuwainua vijana na wanawake kwenye sekta ya kilimo kama ilivyo moja ya agenda kwenye mkutano wa FAO wa mwaka 2023”.
Ameyasema hayo jana (Jumatano, Oktoba 18, 2023) alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ofisi za Makao Makuu ya FAO zilizopo Rome, Italia. Waziri Mkuu yuko nchini Italia akimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023.
Aidha, Mkurugenzi huyo amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na kuboresha mahusiano na mashiriki ya kimataifa.
Dkt. Dongyu ameahidi kutembelea Tanzania mwaka 2024 kwa ajili ya kujionea maendeleo katika sekta ya kilimo pamoja na kupanua wigo wa majadiliano kati ya Tanzania na Shirika hilo ili kuendelea kuwezesha zaidi sekta ya kilimo na uchumi wa Buluu.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema kwa sasa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza kupanua wigo wa kilimo kutoka cha kutegemea mvua na kujikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji, ambapo imetenga shilingi bilioni 900.
“Kilimo ndio maisha, kilimo ndio chakula, tunataka kujikita zaidi katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia mabwawa yetu/ Tunataka tujiridhishe kuwa hakuna Mtanzania atayekufa kwa kukosa chakula.”
Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali inaendelea kufanya maboresho katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na kuhakikisha kinasimamiwa kwa kiwango cha juu ili kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya ndani na ziada kuuza nje.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema kuwa mbali na maboresho hayo yaliyofanyika katika sekta ya kilimo, pia Serikali inawasimia wakulima kuanzia hatua za awali za maandalizi ya mashamba hadi kwenye utafutaji wa masoko kupitia maafisa ugani ambao wapo hadi vijijini.
Pia, Waziri Mkuu Alisema Serikali imeanza kusajili wakulima katika mfumo wa kidigitali lengo ni kujua idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba pamoja na aina ya mazao wanayolima ili kurahisisha ufikishwaji wa huduma za ugani kwa wakati zikiwemo pembejeo. “Usajili huo hautaishia kwa wakulima pekee bado utaendelea hadi kwa wavuvi, wafugaji pamoja na watumiaji wote wa ardhi.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kuishukuru FAO kwa uamuzi wake wa kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa mpango wa BBT ambao unalenga kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki katika kilimo chenye tija.
wa Mataifa la Chakula na Kilimo, (FAO), Dkt. Qu Dongyu baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika kwenye makao makuu ya shirika hilo , Rome nchini Italia Oktoba 18, 2023. Mheshimiwa Majaliwa anamuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani linalofanyika makao makuu ya FAO kuanzia Oktoba 16, 2023 hadi Oktoba 20, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)