Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha ,inatarajia kujenga soko kubwa na la kisasa kwa ajili ya wakazi wa mji wa Mlandizi ambalo litagharimu kiasi cha sh. bilioni saba.
Hayo yalisemwa Mlandizi na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo wakati wa kuhitimisha kampeni ya Simika Bendera kwenye Jimbo hilo.
Mwakamo alisema kuwa eneo maarufu kama kwa Mama Salmini tayari limeshapatikana baada ya kununuliwa na mkandarasi wa ujenzi amepatikana na utaratibu unaanza kwa ajili ya ujenzi.
“Soko la sasa ni dogo lakini eneo tulilopata ni kubwa na litachukua wafanyabiashara wengi na litakuwa na huduma nyingi tofauti na la sasa ambalo hata sehemu ya magari kupaki hakuna,”alisema Mwakamo.
Alisema fedha hizo zimetengwa kwenye baheti ya mwaka wa fedha 2023/2024 na tayari bilioni mbili zimetolewa kwa ajili ya kuanza kazi na litaubadilisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlandizi.
“Nafikiri eneo lilipokuwa soko la zamani likiondolewa iwe stendi ingependeza sana badala ya kuweka vitu ambavyo hazitakuwa na maslahi ya wengi lakini hili la stendi tutaamua kwenye baraza la madiwani,”alisema Mwakamo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini Mkali Kanusu alisema kuwa chama kinataka viongozi waliopo kwenye madarakani wawe na mahusiano mazuri na wananchi.
Kanusu aliwataka wenyeviti wa vitongoji na vijiji kutowalipisha gharama wananchi wanapokwenda kupata huduma kwenye ofisi zao na wale ambao hawaendani na kasi wajirekebishe.
Kwa upande wake katibu wa CCM Kibaha Vijijini Zainabu Mketo alisema kuwa hamasa ya Simika Bendera imeleta mafanikio kwani wamevuna wanachama wapya 3,500 na kupitia mabalozi wote lengo likiwa ni kuimarisha chama ndani ya chama.
Mketo alisema kuwa hamasa ya simika bendera ni kujamasishana kujiandaa na uchaguzi wa vijiji na vitongoji 2024 na uchaguzi mkuu 2025, kuhamasisha ulipaji ada na kuhamasisha wanachama kujisajili na kuelezea yanayofanywa na serikali.