Na Mwandishi Wetu-DODOMA
TAASISI ya WAJIBU iliyoanzishwa kwa lengo la kukuza mazingira ya Uwajibikaji na utawala bora nchini,imeandaa kikao kazi cha siku tatu cha uchambuzi wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) 2021/22 jijini Dodoma.
Kikao kazi hicho kilichowajumuisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini vya kitaifa na vya kijamii pamoja na wadau kutoka taasisi zisizo za kiserikali kimeanza tarehe 17 mpaka 19 Oktoba,2023.
Lengo la kikao hicho ni kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari na Wadau kutoka taasisi zisizo za kiserikali zinazofanya kazi katika ngazi ya Halmashauri kufanya uchambuzi wa kisekta na kutengeneza brosha kwa ajili ya kuongeza utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2021/22
Taasisi ya WAJIBU imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali ikiwemo uchambuzi wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa lugha rahisi na rafiki kila mwaka.