Mwandishi wetu.Arusha.
Taasisi ya Wanahabari ya kusaidia Jamii za pembezoni (MAIPAC) imeeleza changamoto za kihistoria za Jamii za pembezoni nchini na kueleza itaendelea kushirikiana na Serikali na wahisani kutatua changamoto hizo.
Akiwasilisha mada katika Jukwaa la NGO za Afrika katika sehemu ya mikutano ya Afrika wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu na Watu (ACHPR) inayoendelea jijini Arusha, Mkurugenzi wa MAIPAC,Mussa Juma amesema changamoto za Jamii za pembezoni Tanzania hazina tofauti sana na ilivyo katika nchi nyingine barani Afrika na Duniani.
Amesema Jamii hizi zipo nyuma kimaendeleo kutokana na sababu za kihistoria na hivyo kushindwa kunufaika na Rasilimali zilizopo katika maeneo yao licha ya uwepo wa jitihada mbalimbali.
“Bado kuna changamoto ya upatikanaji wa Huduma muhimu kama Elimu,Maji,Afya lakini ardhi ya Jamii hii kuendelea kupungua na kuvamiwa,” amesema.
Amesema MAIPAC kwa kushirikiana na Taasisi za kimataifa, Serikali, Asasi nyingine za kiraia ikiwepo OJADAC, mtandao wa watetezi wa Haki za Binaadamu (THRDC) na nyingine wameendelea kusaidia Jamii hizi.
Hivi karibuni MAIPAC ilikamilisha mradi wa Uhifadhi wa Mazingira, Misitu na Vyanzo vya Maji kwa kutumia maarifa ya asili ambayo ulidhaminiwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia program ya miradi midogo ya shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
Katika mradi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mazingira,Dk Seleman Jaffo alizindua kitabu cha maarifa ya asili katika uhifadhi wa mazingira, Misitu,Vyanzo vya maji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia nchi.
MAIPAC pia inaendelea na mradi wa kukabiliana na ukeketaji,Ndoa za Utotoni na kujengea uwezo kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya Tabia nchi.
Juma amesema, katika kukabiliana na changamoto za Jamii za pembezoni alitaka kuwepo na mkakati wa pamoja kuondoa changamoto hizo.
“Ni muhimu kusaidia jamii hizi kukabiliana na changamoto na ziweze kunufaika na Rasilimali zao za asili ikiwepo ardhi kama ilivyo kwa Jamii nyingine,” amesema.
Amesema MAIPAC itaendelea kushirikiana na asasi nyingine kusaidia jamii hizi ili kuweza kuboresha maisha Yao na kupata fursa zote za kiuchumi na kukabiliana na ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Lakini pia MAIPAC kwa kushirikiana na OJADAC, THRDC, Defend Defenders wamekuwa na mafunzo juu ya masuala ya ulinzi na usalama katika mitan (Digital security and safety) kwa wanahabari na jamii hizi ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza,” amesema.
Amesema ni muhimu Jamii hizi kushirikishwa ipasavyo katika mipango yote inayotekelezwa na katika maeneo yao ili kuondoa migogoro hasa ya ardhi.
Awali, akitoaada katika jukwaa hilo, mtaalam masuala ya haki katika jamii zilizotengwa katika masuala mbalimbali (CDWD) Queen Bisseng amesema jamii za pembezoni barani Afrika zinakabiliwa na changamoto nyingi.
Bisseng amesema Utafiti ambao umefanywa katika nchi kadhaa barani Afrika umebaini Jamii za pembezoni zinakabiliwa na changamoto za kibaya,elimu,Maji na kupokonywa ardhi.
Kamishna wa haki za Binaadamu katika kundi la Jamii za pembezoni Litha Musyimi-Ogana amesema Kamisheni hiyo inatambua changamoto za Jamii hizo.
Akizungumzia ziara ya Tume ya Kamisheni ambayo walifanya Tanzania alisema taarifa rasmi itatolewa hivi karibuni.