Jengo la kufuliwa nguo cha wagonjwa katika kituo cha afya Mbangamao Halmashauri ya mji Mbinga wilayani Mbinga.
Majengo pacha ya upasuaji na jengo la akina mama katika kituo cha afya Mbangamao Halmashauri ya Mji Mbinga yakiwa yamekamilika kwa asilimia zaidi ya 98.
miongoni mwa majengo yaliyojengwa katika kituo cha afya Mbangamao Halmashauri ya Mji Mbinga kama linavyoonekana.
Baadhi ya akina mama wa kutoka kijiji cha Lifakala Halmashauri ya Mji wakiwa na ndoo za kubeba mchanga kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya mkiundombinu inayojengwa katika kituo cha afya Mbangamao.
Na Muhidin Amri,
Mbinga
WANANCHI wa kata ya Mbangamao Halmashauri ya mji Mbinga mkoani Ruvuma,wanakwenda kuondokana na adha ya kutembea umbali wa kilomita 25 hadi Mbinga mjini kufuata huduma za afya kufuatia ujenzi wa kituo cha afya Mbangamao kufikia asilimia 98 ya ujenzi wake.
Baadhi ya wananchi waliokutwa wakishiriki ujenzi huo kwa kusogeza tofari na mchanga,wameishukuru serikali kupitia Halmashauri ya mji Mbinga kuona umuhimu wa kujenga kituo hicho ambacho kitawezesha kupata huduma za afya karibu na makazi yao .
Dustan Ndunguru alisema,kumalizika kwa mradi huo kutarahisisha na kusogeza karibu huduma za afya kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani na kupunguza vifo hasa kwa akina mama wajawazito na watoto.
Ndunguru ambaye ni mjumbe wa kamati ya ujenzi, ameiomba Serikali kupeleka wafanyakazi(wauguzi na madaktari) watakaofanya kazi katika kituo hicho kwa kuwa ujenzi wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 98 ili wananchi waweze kupata huduma za afya.
Hata hivyo,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kutoa fedha za mradi huo na kuwapongeza wataalam wa Halmashauri ya Mji Mbinga kwa ushauri na usimamizi uliosaidia kazi ya ujenzi kufanyika kwa weledi na ubora wa hali ya juu.
Rose Komba, mkazi wa kijiji cha Lifakara alitaja changamoto zinazowakabili kwa sasa ni kukosekana kwa baadhi ya huduma muhimu katika zahanati ndogo iliyojengwa tangu miaka ya themanini zikiwemo vipimo vya damu,magonjwa ya zinaa,upasuaji mdogo na mkubwa pamoja na watumishi wenye sifa.
Alitaja changamoto nyingine kwa mama wajawazito pindi wanapotakiwa kujifungua kulazimika kwenda hadi Hospitali ya wilaya Halmashauri ya Mji (Mbuyula)iliyopo Mbinga mjini kwa kutumia usafiri wa boda boda ambao siyo salama kwa wajawazito.
Kwa upande wake mfamasia wa kituo cha afya Mbangamao Simon Njako alisema,kituo kitakapokamilika kitahudumia watu wengi na kutoa huduma nyingi tofauti na huduma zinazotolewa kwa ngazi ya zahanati.
Aidha alisema,wagonjwa wengi wanaofika kutibiwa kwenye zahanati wanasumbuliwa na mfumo wa hewa hasa watoto wadogo na wanashindwa kuwahudumia kutokana na uhaba wa vitendea kazi.
Alitaja ugonjwa mwingine ni kifua kikuu ambao kwa ngazi ya zahanati hakuna vipimo kwa ajili ya kufanyia uchunguzi ,badala yake wanalazimika kuchukua sampuli za makohozi na kupeleka Hospitali ya mji Mbinga na hivyo kuathiri sana mkakati wa serikali wa kusogeza huduma karibu kwa wananchi.
Kwa upande wake kaimu mganga mkuu wa Halmashauri ya mji Mbinga Maximo Magehema alisema,kwa sasa kazi zinazoendelea ni kufung milango,vifaa vya umeme na maji wakati wanasubiri vifaa tiba kutoka MSD.
Alisema,ujenzi wa kituo hicho umegharimu kiasi cha Sh.milioni 500 zilizotolewa na Serikali kuu na kitakapokamilika huduma zitakazotolewa ni huduma ya upasuaji, kuongezewa damu na huduma nyingine ambazo hazipatikani kwa ngazi ya zahanati.