Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya Mwachembe Mjeni aliyein ma,akiwaonyesha wajumbe wa kamati ya ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Simambwe kata ya Tembela baadhi ya miundombinu iliyojengwa katika mradi huo.
Mhandisi wa maji kutoka ofisi ya meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) Felix Msangi kulia,akizungumza na wajumbe wa kamati ya ujenzi wa mradi wa maji wa Simambwe na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wake.
Tenki la kuhifadhi lita 250,000 za maji litakalohudumia vijiji vinne kikiwemo kijiji cha Simambwe Halmashauri ya wilaya Mbeya likiwa katika hatua za mwisho kukamilika.
Na Muhidin Amri,
Mbeya
ZAIDI ya wakazi 6,994 wa vijiji vinne vya
Ilembo usafwa,Simambwe,Shiboliya na Usoha njiapanda Halmashauri ya wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya,wanatarajia kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kufuatia wakala wa maji na usafi wa mazingira(Ruwasa)kuanza kutekeleza mradi wa maji wa Simambwe.
Mradi huo umetengewa kiasi cha Sh.milioni 636 zitakazotumika kumaliza shida ya maji katika vijiji hivyo,ambavyo kwa muda mrefu wakazi wake wanatumia maji yanayopatikana kwenye mabonde na visima vya asili ambayo siyo safi na salama kwa kuwa yanatumika pamoja na wanyama wa kufugwa.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbeya Mwachembe Mjeni alitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa tenki la lita 250,000 vituo vya kuchotea maji 31,kulaza mabomba ya kusambaza maji kutoka kwenye chanzo hadi kwa wananchi umbali wa mita 17,500.
Mwachembe alisema,hadi sasa kazi zilizofanyika ni ujenzi wa tenki,ujenzi wa chanzo(banio)kulaza mabomba urefu wa mita 11,000 kutoka kwenye chanzo hadi lilipo tenki na kwenda kwenye makazi ya wananchi .
Aidha alisema,mradi haujakamilika kwa muda uliopangwa kutokana na kuchelewa kwa fedha kutoka serikalini,hata hivyo fedha zimefika na mkandarasi ameshalipwa kiasi cha Sh.milioni 402 kati ya Sh.milioni 636.
Mwenyekiti wa kijiji cha Simambwe Michael Mwanyanje alisema,serikali ilihaidi kukamilika mradi huo mwezi Novemba mwaka jana,lakini mpaka sasa bado haujakamilika na haujakabidhiwa kwa wananchi ambao wanaendelea kuteseka kwa kukosa huduma ya maji.
Mkazi wa kijiji hicho Florian Msika alisema,serikali ilipotangaza kijiji hicho kitapata mradi wa maji ya bomba walishukuru na walishiriki kwa kuchimba mitaro kwani waliamini wataondokana na adha ya kutembea umbali wa kilomita mbili kila siku kwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili.
Alisema,hata hivyo wananchi wanaona kama wamedanganywa kwani ni zaidi ya miezi 11 mradi haujakamilika na kuiomba serikali kupitia Ruwasa kuwa karibu na kumbana mkandarasi ili akamilishe kazi na wananchi wapate maji safi na salama karibu na makazi yao.
Velelian Sanga,amemtaka mkandarasi kuongeza nguvu katika ujenzi wa mradi huo ili aweze kukamilisha kazi zilizopangwa kabla ya kuanza kwa mvua za masika ambazo zinaweza kusababisha kazi kusimama kwa muda mrefu.