Muonekano wa nyumba ya mashine ya kuvutia maji(Pump House)iliyojengwa kupitia mradi wa maji Sangambi Halmashauri ya wilaya Chunya mkoani Mbeya kwa gharama ya zaidi ya Sh.milioni 5.
Mwenyekiti wa mradi wa maji wa Sangambi wilaya ya Chunya mkoani Mbeya Flora Ndukwa kushoto akimtwishwa ndoo ya maji mkazi wa kijiji hicho ambaye hakutaka kutaja jina lake wakati ukaguzi wa miundombinu ya mradi huo.
Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000 za maji ambalo linahudumia zaidi ya wakazi 6,779 wa kijiji cha Sangambi wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.
Na Muhidin Amri-Chunya
WAKALA wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),imefanikisha kumaliza kero ya muda mrefu ya huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa kijiji cha Sangapi Halmashauri ya wilaya Chunya mkoani Mbeya baada ya kujenga wa mradi mkubwa wa maji.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilayani Chunya David Nyambulapi alisema,mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 507 kwa kumtumia mkandarasi chini ya usimamizi wa ofisi ya meneja wa Ruwasa wilaya ya Chunya na umeanza kutoa huduma kwa wakazi zaidi ya 6,779 wa kijiji hicho.
Alitaja kazi zilizofanyika ni kuchimba kisima chenye uwezo wa kuzalisha lita 12,000 kwa saa,uvutaji wa umeme umbali wa kilomita 1.2,ujenzi wa vituo sita vya kuchotea maji,uchimbaji wa mitaro na kulaza bomba urefu wa kilomita 23.
Kwa mujibu wa Nyambulapi,kazi nyingine zilizotekelezwa ni kujenga nyumba ya mashine(pump house) kujenga uzio eneo la tenki na kujenga tenki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 150,000 ambalo linatoshelesha kuhudumia wakazi wa kijiji hicho chenye shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo uchimbaji wa dhahabu.
Aidha alisema,katika uendeshaji wa mradi huo changamoto kubwa ni kukatika mara kwa mara kwa umeme ambao umeathiri mpango wa Ruwasa kufikisha huduma bora ya maji kwa wananchi.
Alisema,wanatumia mashine kusukuma maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye vituo vya kuchotea maji,hivyo kupsababisha upungufu wa maji kwa baadhi ya maeneo.
Katika hatua nyingine Nyambulapi alisema,serikali imetoa kiasi cha Sh.milioni 100 kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji safi na salama kwa baadhi ya maeneo/vitongoji ambavyo bado haijafikiwa na huduma hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Sangambi Junjulu Mhewa,ameishukuru serikali kuipatia fedha Ruwasa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao umesaidia kumaliza changamoto ya maji katika kijiji hicho na maeneo mengine wilayani Chunya.
Alisema,kabla ya mradi huo wananchi wa kijiji hicho walilazimika kutembea umbali wa masaa mawili hadi matatu kwenda kutafuta kwenye makalongo na visima vilivyochimbwa na wananchi wenyewe.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Sangambi Lusekelo Lwesya,ameiomba serikali kufikisha huduma ya maji kwenye vitongoji vikiwemo vya Izumbi ambavyo havijafikiwa na mtandao wa maji ya bomba.
Naye mwenyekiti wa mradi wa maji Sangambi Flora Ndukwa alisema,mgao wa umeme umechangia kurudisha nyuma jitihada za kutoa huduma ya maji, kwani tenki linalotumika kusambaza maji kwenda kwa wananchi halipokei maji ya kutosha kutoka kwenye chanzo.
Ameiomba serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),kutafuta ufumbuzi wa kero hiyo ambayo imeathiri upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Mkazi wa kijiji cha hicho Maneno Ngaponda,ameshauri wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha wanajaza maji ya kutosha kwenye tenki pindi umeme unapowaka ili kuepuka upungufu wa maji.