Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage ameeleza, kiasi cha sh. BIln 15 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Alitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika mjini Kibaha, kikihusisha viongozi na watendaji wa wilaya,mkoa na Tanroads na TARURA wa Wilaya, Wakurugenzi na viongozi wengine wa mkoa huo.
Alisema hadi kufikia robo ya mwaka wa fedha 2023/2024 sh. Miln 18.3 zimepokelewa katika mkoa huo kuendelea na shughuli mbalimbali za miradi ya barabara.
Meneja huyo alibainisha kwamba katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 bajeti ya mkoa imeongezeka sh. Biln 10.811 katika fedha za miradi ya maendeleo.
Mhandisi Mwambage alieleza vikwazo wanavyokutana navyo kuwa ni pamoja na wizi, uharibifu wa thamani za barabara na uvamizi wa hifadhi.
Pia alieleza kuwepo kwa malalamiko kutokana na ucheleweshaji wa malipo ya fidia sehemu zilizofanyiwa tathmini
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge alizitaka TANROADS na TARURA kutengeneza barabara kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji muhimu ili kuondoa vikwazo vya kutopitika muda wote.