Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,Abubakari Kunenge ametoa Rai kwa watendaji kusimamia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa wakati kwa maslahi ya wananchi.
Aidha alizitaka Halmashauri ziache kuwa ombaomba kwa wawekezaji na kuwatafutia vikwazo vya kisheria hali inayosababisha kuwapa maumivu.
Akizungumza na viongozi pamoja na watumishi na watendaji wa mkoa na wilaya katika kikao Cha ushauri Cha mkoa (RCC) alisema , Serikali inatenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hivyo bila kuisimamia itakuwa tunamuangusha Rais Samia Suluhu Hassan.
Alieleza, Rais anafanya juhudi kubwa kuleta fedha za miradi ya maendeleo akiamini ,miradi inasimamiwa na kumalizika kwa wakati ili ilete tija kwa wananchi.
Awali Katibu Tawala msaidizi Mipango na Uratibu Mkoani Pwani, Edina Katalaiya alisema ,Mwaka 2022/2023 mkoa uliidhinishiwa bajeti ya Bilioni 335.110.4 kati ya fedha hizo bilioni 286.632.1 ni kwa ajili ya ruzuku ya matumizi ya kawaida na maendeleo na sh Bilioni 48.478.338 za mapato ya ndani ya Halmashauri.
Kati ya fedha za ruzuku sh.206.063.824.0 za mishahara na matumizi mengineyo na sh.80.568.294.0 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Vilevile Edina alieleza, mwaka 2022/2023 jumla ya sh.bilioni 249.155.581.144 kati ya sh.286.632.118.0 zilipokelewa sawa na asilimia 86.93 ya bajeti ya fedha za ruzuku.
Kati ya kiasi hicho sh.185.961.021.205.45 zimelipwa mishahara,sh.bilioni 13 .321.828.822.08 za matumizi mengineyo ( OC ),na sh.53.499.163.545.26 za maendeleo”.
Edina alitaja baadhi ya Changamoto kuwa ni katika utekelezaji wa bajeti 2022/2023 ni pamoja na ufinyu na ukomo wa bajeti usiotosheleza mahitaji ukilinganisha na jiografia na ukubwa wa mkoa kutoka eneo moja kwenda lingine,uwepo wa visiwa na delta ya mto Rufiji hali inayofanya gharama za uendeshaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuwa kubwa.
Upungufu na uchakavu wa miundombinu ya kutolea huduma za elimu na afya, upungufu wa watumishi hasa kada za afya,elimu walimu wa hesabu, sayansi na maafisa ugani katika halmashauri.