Wakazi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuwa mstari wa mbele kulinda miundombinu ya barabara zinazo jengwa katika maeneo yao ili ziweze kutumika kwa muda mrefu kuchochea shughuli za maendeleo kama ilivyo lengwa pia kufichua wanaohusika kuhujumu miundombinu hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni ametoa rai hiyo akizingumza na wakazi wa Kilangare baada ya kukagua Barabara zinazojengwa wilayani humo na kutambulisha kwa wananchi wakandarasi waliopewa kazi na serikali kujenga barabara kwa kipindi cha mwaka 2023-2024 akisema ni wajibu wa wananchi kulinda barabara hizo ziweze kuwanufaisha kiuchumi .
“Nisingependa kuona barabara zinaharibiwa , Alama za barabarani zinatolewa lakini pia vifaa vinavyotumiwa na wakandarasi katika ujenzi wa barabara hizo ni jukumu letu wananchi kuhakikisha vinalindwa”.Alisema mkuu huyo wa Wilaya.
Pia amewataka wakandarasi kutoa ajira ndogo ndogo zisizohitaji utaalam kwa wananchi wa maeneo ambayo barabara zinajengwa na pia kuwapa taarifa za maendeleo ya mradi pale wananchi wanapohitaji taarifa hizo .
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Mhe.Anne Kilango Malecela ameiomba Serikali kuwaongezea fedha wakala wa Barabara Mjini na Vijijini TARURA Wilayani humo kuwezesha kujenga daraja kuunganisha kata ya Kirangare na Mpinji.
Amesema bado wananchi wa Kirangare ambao wanategemea soko la Myamba hawataweza kuvuka upande wa pili hadi daraja hilo litakapokuwa limejengwa hivyo kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha kuwezesha mawasiliano baina ya pande hizo mbili.
Hata hivyo nitakuwa mchoyo wa fadhira nisipotoa shukran kwa Mhe. Rais mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassani kuendelea kuwathamini wananchi wake kwa ujenzi wa barabara hii ya Idaruu-Narema tunayo itambulisha kwenu ambayo itaghalimu takribani shilingi Million 395
Meneja wa TARURA Wilaya ya Same Mhandisi James Mnene amesema barabara hiyo yenye urefu wa Km 7 inayojengwa kwa kiwango cha changarawe inagharimu Jumla ya shilingi Milioni 395 ambazo ni fedha za tozo.
Kuhusu Ujenzi wa daraja la kuunganisha Kata hizo mbili Mhandisi Mnene amesema TARURA itafanya tathimini kujua gharama halisi za Ujenzi wake na kuwasilisha TARURA Mkoa kwaajili ya kuomba fedha za Ujenzi kwakua daraja hilo lina umuhimu mkubwa.