**
Mwanza. Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yamechangia ongezeko la watu wanaotegemea vifaa ikiwemo Kompyuta na Simu katika shughuli za uzalishaji.
Kutokana na matumizi ya kupindukia ya vifaa hivyo, baadhi ya watumiaji wamejikuta wakipata madhara ikiwemo kupata maradhi ya macho huku wengine wakipata upofu kutokana na macho kuathirika kwa muda mrefu.
Kutokana na uwepo wa changamoto hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dk Fabian Massaga ametaja mbinu ya ’20-20-20′ kuwa inaweza kutumika kulinda afya ya macho kwa wanaotumia vifaa ikiwemo simu na Kompyuta kwa muda mrefu.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya macho duniani iliyofanyika leo Bugando, Dk Massaga ametoa tafsiri ya mbinu hiyo kuwa ni mtumiaji wa Kompyuta kufuata sheria ya 20-20-20 ambayo inamtaka mlengwa kila baada ya dakika 20 kutazama umbali wa futi 20 kwa sekunde 20.
“Kufanya hivyo kwa kujirudia rudia kunawezesha mishipa ya macho ipumzike na kurejea katika hali yake ya asili. Lakini usipofanya hivyo unajitengenezea uwezekano mkubwa wa kuugua macho yako,” amesema Dk Massaga.
Katika hatua nyingine Dk Massaga ametaja visababishi 10 vinavyochangia maradhi ya macho ikiwemo uvutaji sigara na matumizi ya kompyuta bila tahadhari.
Sababu nyingine ni matumizi ya vipodozi vilivyoisha muda wake, miwani ya kusomea bila kushauriwa ama kuthibitishwa na watalaam, kutokula chakula bora kinachosaidia kurutubisha afya ya macho, kutofanya mazoezi na kutobadilisha blashi za kusafishia uso.
Pia kutokuwa na utamaduni wa kupima macho na watoto kutopata muda wa kucheza nje kuwasaidia kuona mbali na badala yake kushinda ndani wakichezea simu za wazazi wao na kutazama runinga.
“Wananchi chukueni tahahari mbalimbali za kukinga macho yasiathiriwe hasa mnapokuwa kwenye shughuli za uzalishaji viwandani, migodini, kilimo, uvuvi, maofisini na uchomeleaji vyuma kwani zimekuwa na madhara ya moja kwa moja kwenye afya ya macho,” amesisitiza.
“Hata watoto wadogo waruhusiwe kushiriki michezo ya nje kunawapa nafasi ya kuona mbali na siyo karibu tu, vaeni miwani ya kukinga miale ya jua na wanaohitaji miwani ya kusomea na kutembelea wavae iliyopimwa na wataalam na kuthibitishwa,” amesema Dk Masanga na kuongeza;
“Wanaotumia vipodozi angalieni muda wake wa matumizi na kumbuka kubadilisha brashi kila mara, tufanye mazoezi kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa yanayoweza kuathiri macho, tule mlo kamili wenye kurutubisha afya ya macho, usivute sigara kwani tafiti zinaonyesha sigara huchangia kuleta magonjwa mbalimbali yakiwamo ya macho, na pima macho yako mara kwa mara hata kama unaona hayana tatizo,”
Awali, akiwasilisha taarifa ya ukubwa wa tatizo la macho hospitalini hapo, Mkuu wa Idara ya Macho Bugando, Dk Christopher Mwanansao, amesema watu 2,500 hutibiwa matatizo ya macho hospitalini hapo kila mwezi
Amesema kupitia wiki ya maadhimisho hayo wamewafanyia upasuaji wagonjwa 32 wenye tatizo la mtoto wa jicho, kutoa ushauri, elimu na vipimo vya shinikizo la macho, miwani ya kusomea na kuwatembelea wafanyakazi katika migodi ya uchimbaji madini mkoani Geita.
“Tumewatembelea na wafanyakazi wa viwanda vya vinywaji Mwanza na Shinyanga. Mnapopata changamoto yoyote ya macho msijitibu nyumbani, fikeni hospitalini mara moja kupata huduma za kitaalam kuliko kukimbilia kwenye maduka ya dawa ambako huwa hawapati huduma sahihi,” amesema
Kwa upande wake Mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, Suzana Steven, amesema amefika hospitali hapo kupata huduma ya uchunguzi baada ya kusumbuliwa na tatizo la huoni hafifu kwa miaka mitatu baada ya kufanya kazi ya katibu muhtasi, huku akishauri wananchi kufuata elimu inayotolewa na wataalam hao kuepuka changamoto za kupata upofu.