NA VICTOR MAKINDA: IFAKARA, KILOMBERO.
Chama cha Mapinduzi CCM, wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kimewataka watendaji wote wa serikali wilayani hapa kuacha uzembe kazini na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuzidi kuwaletea maendeleo wananchi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilombero, Mohamed Msuya, alipozungumza na Fullshangweblog mjini Ifakara wilayani Kilombero jana.
Msuya alisema kuwa wapo baadhi ya watendaji wa serikali wilayani hapa ambao wanafanya kazi kimazoea na kuendekeza urasimu ambao huchelewesha utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi na kudumaza maendeleo.
“ Ninawaonya watendeji walio katika ajira za serikali wilayani Kilombero, ambao hawaendani na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan , katika kutatua changamoto za wananchi, waiache tabia hiyo haraka na wajikite katika kufanya kazi kwa weledi, bidii na maarifa kulingana na mikataba yao ya ajira zao.” Alisema Msuya.
Msuya aliongeza kuwa watendaji magoigoi wataifanya CCM kuchukiwa na wananchi kwa kuwa chama hicho ndicho kilichoaminiwa na kuchaguliwa kuangoza serikali.
“ CCM Kilombero tumejidhatiti kuhakisha ilani ya chama inatekelezwa kwa asilimia mia hiyo watendaji wa serikali wa kada zote, wanaofanya kazi kwa ugoigoi watachukuliwa hatua ili wasiwe chanzo cha kutukwamisha kutekeleza ilani ya uchaguzi na hatimae kukataliwa na wananchi.” Alisema.
Msuya aliongeza kusema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imepeleka miradi mingi ya maendeleo ikiwemo afya, miundombinu, elimu na maji wilayani Kilombero, hivyo watendaji wa serikali wilayani humo wanapaswa kusimamia miradi hiyo kikamilifu ili ilete tija inayokusudiwa kwa wananchi.
Akizungumzia uimara wa chama hicho, Msuya alisema kuwa CCM wilayani Kilombero ipo imara na inaendelea kusimamia utekelezaji wa ilani yake ambapo kwa sasa imeelekeza nguvu katika ujenzi wa miundombinu ya chama hicho ikiwa imepanga kujenga ofisi ya wilaya, nyumba za watendaji wa chama na Jumuiya zake ngazi ya wilaya na kukarabati uwanja wa mpira unaomilikiwa na chama hicho uliopo mjini Ifakara.
“Uimara wa CCM unategemea sana na watenadaji waliojitoa kufanya kazi kwa ufanisi na ubora wa miundombinu ya utolewaji wa huduma. Kwa sasa tupo katika mopango kabambe wa kuimarisha miundombinu ya chama hivyo tunawaomba wadau wote wa maendeleo wa wilaya ya Kilombero, walio nje na ndani ya nchi, tusaidiane kwa pamoja kutimiza azma hii ya kujenga miundombinu bora ya kisasa kwa ajili ya kukiimarisha chama chetu kiweze kuendelea kutoa huduma bora”. Alisema Msuya.