NA STEPHANO MANGO, MBINGA
KAMATI ya Siasa Mkoa wa Ruvuma imeridhishwa na utekelezeaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Hata hivyo imemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuongeza kasi katika utekelezaji huo ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuleta tija kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa jana na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma Mohamed Ally katika ziara ya Kamati ya Siasa Mkoa wa Ruvuma iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita
” Tumetembelea miradi na tumeona utekelezaji wake, Mkurugenzi endeleza ari hiyo ili miradi hii itekelezwe katika ubora na viwango tarajiwa ili Wananchi waweze kunufaika na dhamira ya dhati ya Rais “Amesema Ndg. Ally
Pamoja na pongezi hizo amewashukuru wananchi wa Kata ya Kipapa kwa kuona haja na kutoa eneo lenye ukubwa wa ekari 5 na nusu kwaajili ya ujenzi wa shule mpya ya Msingi Kilango.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbinga Joseph Mdaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
” Kipekee sana nimshukuru Rais wetu Dkt Samia Hassan Suluhu kwa kutuona wana Mbinga na kutuletea fedha nyingi kwaajili ya utekelezaji wa miradi hii tunashukuru sana” Amebainisha Mdaka