MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon amesema ili kuondokana na kikwazo cha ukosefu wa maji kwenye baadhi ya maeneo Jamii inatakiwa kujenga tabia ya kulinda vyanzo vya maji badala ya kuacha kazi hiyo kufanywa na Serikali pekee.
Saimon amesema kila mmoja anatakiwa kwenye eneo lake kuwa mlinzi wa vyanzo vya mqji sambamba na miundombinu inayojengwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Amesema suala la maji likiachwa kwa Serikali peke yake ni kutengeneza jamii ambayo haina uwajibikaji ili hali kila mmoja anatakiwa katika eneo lake kulipa bili kwa wakati, kulinda vyanzo vya maji na kutoa taarifa inapotokea hitilafu.
Mkuu huyo wa Wilaya aliyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha nusu mwaka cha wadau wa sekta ya maji kilichoandaliwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Kibaha Mhandisi Debora Kanyika amesema kwasasa huduma ya maji imeimarika na tayari vijiji 25 kati ya 26 vimefikiwa.
Mhandisi Debora amesema miradi yote iliyokamilika inawanufaisha watu 100,220 na kuinua hali ya upatikanaji wa maji kwa miaka 11 na kupelekea ongezeko la wanaopata huduma ya maji kufikia asilimia 78 kutoka 67 ya mwaka 2019.
Kwa mujibu wa Meneja huyo ifikapo June 2024 asilimia ya wakazi wa Kibaha Vijijini watakuwa na huduma ya maji safi na salama kupitia uteekelezaji wa miradi ya bajeti ya mwaka huu.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho ambaye ni Diwani Viti Maalumu Josephine Gunda ameomba Mamlalka hiyo kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya miradi mikubwa iliyokamilika ili marekebisho yaendelee kufanyika maeneo yenye vikwazo.
Gunda pia ameomba RuWASA kuzingatia idadi ya wanufaika kwenye maeneo wanayounganisha maji ili yakidhi mahitaji sambamba na kuyafikisha maeneo ya Vitongoji.
Naye Kalshinde Juma ameomba nishati ya umeme iunganishwe kwenye miradi ya maji ili yapatikane muda wote kwani sehemu wanayotumia sola maji hayawezi kupatikana nyakati zote hususani usiku.