Na Lucas Raphael,Tabora
Jeshi la Polisi wilaya ya Igunga mkaoni Tabora limemfikisha katika Mahakama ya hakimu mfawidhi wilaya ya Igunga, Hamis Said(37) mkazi wa mtaa wa Nkokoto, kata ya Igunga mjini kwa tuhuma ya kumpa ujauzito mwanaye (jina limehifadhiwa) anayesoma kidato cha pili katika shule ya sekondari Igunga mjini mwenye umri wa miaka 16.
Awali mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya mkuu wa mashitaka wilaya ya Igunga Albanus Ndunguru aliiambia mahakama mbele ya hakimu wa wilaya ya Igunga, Edda Kahindi kuwa mshtakiwa huyo anashitakiwa kwa tuhuma ya makosa mawili.
Nduguru alisema shitaka la kwanza linalomkabili mshtakiwa Hamisi Said ni kufanya mapenzi na mwananye kinyume na kifungu 158 kidogo cha cha kwanza cha sheria ya kanuni ya
Adhabu sura ya 16 mapitio ya 2022.
Alisema kati ya mwaka 2018 tarehe tofauti hadi Juni 2023 mshtakiwa alitenda kosa la kufanya mapenzi na mwananye
Nduguru alisema shitaka la pili linalomkabili mshtakiwa Hamis Said ni kumpa ujauzito mwanafunzi anayesoma kidato cha pili shule ya sekondari Igunga mjini mwenye umri wa miaka 16 (jina limehifadhiwa)
Alisema Juni 2023 mshtakiwa huyo alimpa ujauzito mwanafunzi ambapo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 60 A kidogo cha tatu cha sheria ya elimu sura 353 ya 2019 inayozuia kutenda makosa kama hayo.
Aidha, mwendesha mashitaka huyo aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo aliomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa hoja za awali.
Hata hivyo, baada ya mshtakiwa kusomewa mashitaka hayo mawili alikana kutenda makosa hayo ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi oktoba, 20, 2023 na mshitakiwa amepelekwa mahabusu baada ya kukosa mdhamini aliyetakiwa kusaini dhamana ya milioni 2.