Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Lukanga akizungumza wakati wa kufungua rasmi warsha ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa. Warsha hiyo inafanyika jijini Dar es Salaam ambapo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utafiti pamoja na Uratibu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Mary Kishe akibainisha umuhimu wa tafiti na kuainisha mafanikio ya taasisi hiyo ambapo mwaka huu inafikisha miaka 40, wakati wa warsha ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini. Warsha hiyo inafanyika jijini Dar es Salaam ambapo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani.
Picha ya pamoja ya washiriki wa warsha ya kufanya tafiti ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa. Warsha hiyo inafanyika kwa siku tano jijini Dar es Salaam ambapo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani ambapo wanafanya tafiti ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.
Na. Edward Kondela
Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ikishirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani inafanya tafiti ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.
Akizungumza (09.10.2023) kando ya warsha hiyo baada ya kuifungua rasmi, inayoendelea jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Lukanga amesema tafiti hizo zitaibua taarifa za maeneo ambayo sehemu ya maziwa na Bahari ya Hindi iliyopo nchini kuweka taarifa zake sahihi kulingana na idadi ya watu ambao wamekuwa wakinufaika kupitia rasilimali zilizopo katika maji hayo.
Bw. Lukanga ameongeza kuwa kwa sasa idadi ya watu nchini imeongezeka na kufikia zaidi ya milioni sitini ila bado taarifa zilizopo kwenye sekta ya uvuvi zinatolewa kulingana na idadi ya watu iliyokuwepo zamani ya zaidi ya milioni 40 ambayo imekuwa ikibainisha watu wanaojishughulisha moja kwa moja katika sekta ya uvuvi ni milioni 4.5.
Aidha, amesema warsha hiyo imeanzishwa na wanasayansi na watafiti kutoka nchi zaidi ya 58 kuhakikisha rasilimali ambazo hazijionyeshi kwa uwazi ziweze kuonekana hususan kwenye uvuvi mdogo ili kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utafiti pamoja na Uratibu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Mary Kishe amesema taasisi hiyo ambayo mwaka huu inafikisha miaka 40 imekuwa ikikusanya na kutafiti masuala mbalimbali ya sekta ya uvuvi lakini bado haijaangalia mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa na mtu mmoja mmoja.
Amesema kupitia warsha hiyo inayoendelea jijini Dar es Salaam, ambapo TAFIRI inashirikiana na FAO pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani wataweza kuunganisha taarifa za zamani na kuziweka pamoja na kuona umuhimu wa takwimu hizo kwa maendeleo endelevu ya sekta ya uvuvi kwa kuwa kuna taarifa ambazo zimejificha ambazo hazionyeshi usahihi juu ya sekta hiyo.
Pia, amesema warsha hiyo ni muhimu ambapo watafiti watapata fursa ya kutoa mapendekezo yao ya namna ya kusimamia rasilimali za uvuvi ili kuweza kufikia lengo la sekta ya uvuvi kuongeza mchango zaidi katika pato la taifa.
Naye Afisa Mkuu kutoka FAO, Bw. Nicolas Gutierrez na Afisa Mipango Mtafiti kutoka FAO Bi. Nicole Franz wakizungumza kando ya warsha hiyo wamesema uwepo wa taarifa sahihi ni muhimu katika kuendeleza sekta ya uvuvi nchini pamoja na kutoa elimu kwa wavuvi wa umuhimu wa taarifa hizo pamoja na kulinda rasilimali za uvuvi.
Wamebainisha pia uwepo wa taarifa sahihi ya sekta ya uvuvi utawezesha kubadili maisha ya watu wanaojishughulisha na uvuvi hususan wavuvi wadogo kwa kuangalia namna wanavyochangia katika sekta hiyo kwa kuwa ni sekta ambayo inachangia katika ongezeko la chakula duniani.
Warsha hiyo ambayo ni muhimu katika kuangalia mchango wa sekta ya uvuvi nchini inafanyika kwa siku tano jijini Dar es Salaam ambapo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani ambapo wanafanya tafiti ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.