Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENGE wa uhuru umezindua mradi mkubwa wa maji wenye kuwanufaisha wakazi 2,12 na mifugo 7,826 kwenye kijiji cha Emboreet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Awali, huduma ya maji ilikuwa inapatikana kwa wakazi wa eneo hilo kwa kutembelea kilomita nne kufuata huduma ya maji yaani kwenda kilomita mbili na kurudi kilomita mbili.
Meneja wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilayani Simanjiro, mhandisi Joanes Martine akisoma taarifa ya uzinduzi wa miradi huo amesema maji yatapatikana ndani ya mita 400 hadi 1,000.
Mhandisi Martin amesema mradi huo wa maji umegharimu Sh292.8 milioni na unaendana na kampeni ya kitaifa ya kumtua mama ndoo kichwani.
“Kati ya fedha hizo Serikali kuu imetoa Sh264.2 milioni kupitia mpango wa uendelevu wa huduma ya maji na usafi wa mazingira vijijini (PforR) Sh26.1 milioni za shirika la OIKOS na Carbon sink na Sh2.5 milioni ni mchango wa jamii,” amesema mhandisi Martin.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2023 Abdalah Shaibu Kaim amesema mwenge wa uhuru umeridhia kuzindua mradi huo wa maji kwenye kijiji cha Emboreet.
Kaim amesema kupitia mradi huo wananchi wa eneo hilo watanufaika kwa kupata maji kwa karibu na kwa manufaa zaidi kwani maji ni uhai.
“Hivi sasa mambo yatakuwa bulbul kwani maji yatapatikana kwa raha zao hivyo tunaipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mradi huu,” amesema.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera amesema mwenge utazindua barabara ya lami Orkesumet, mradi wa mazingira na usafi sokoni.
Dk Serera amesema utatembelea hospitali ya wilaya jengo la wagonjwa mahututi Kata ya Langai na kuzindua shule mpya ya Msingi ya Lengijape kijiji cha Namalulu kata ya
Naberera.
Amesema utazindua josho la Ormoti na kuzindua mradi wa maji kijiji cha Emboreet na kuweka jiwe la msingi jengo la wagonjwa wa nje kituo cha afya Loiborsiret.
“Baada ya hapo mwenge wa uhuru utakagua vikundi vya wajasiriamali, kutembelea mabanda na mkesha katika uwanja wa mpira wa shule ya msingi Loiborsiret,” amesema Dk Serera.