Na Mwandishi wetu – Mwanza
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayehusika na Elimu, Dkt. Franklin Jasson Rwezimula leo Oktoba 7, 2023 ametembelea Taasisi ya Tekenolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza kuona Maendeleo ya shughuli za ujenzi wa Kituo cha Umahiri wa Teknolojia ya Ngozi (Center of Excellence) na kumtaka mkandarasi aongeze kasi ya ujenzi huo.
Ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa ujuzi kwa maendeleo na uingiliano wa kikanda katika Ukanda wa Afrika Mashariki (EASTRIP), unaotekelezwa na serikali kwa Ufadhili wa Benki ya Dunia.
Dkt. Franklin ametoa agizo hilo alipotembelea Mradi na kukuta kasi ya mkandarasi haiendani na makubaliano ya awali ya kukamilisha na kukabidhi mwezi Desemba mwaka huu.
“Sisi kama serikali pesa yote tumeshamlipa, hivyo anapaswa kukamilisha kazi hii kwa wakati. kituo hiki Cha Umahiri wa Teknolojia ya Ngozi kitakapokamilika kitakuwa msaada mkubwa ndani na nje yaTanzania kwa kuwa kitaongeza wataalam wa masuala ya Ngozi, kufundisha wakulima na wafugaji pamoja na kuchakata mazao ya ngozi”,amesema.
Kwa upande wake Mhandisi Mshauri na msimamizi wa mradi upande wa serikali Silvester Francis amesema hadi sasa mradi huu umekamilika kwa asilimia 60% na amebainisha maeneo ambayo yamekamilika jengo la taaluma, utawala, mabweni ya kiume na kike, jengo la ngozi ( Leather Building) na uzio.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa DIT-Mwanza ambae pia ni kaimu Mratibu wa mradi wa (EASTRIP) Mhandisi Issa Mwangosi amekiri kupokea maelekezo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu (Elimu) ya kumsimamia mkandarasi aongeze kasi ya ujenzi ili akamilishe ujenzi huo kwa wakati kama ilivyopangwa kwenye Mkataba.
Mradi huo ulianza kutekelezwa Mwaka 2019 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2024 ambapo utagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania Bilioni 37.