Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatirio akikabidhiwa vifaa vya hospitali ya wilaya ya Tunduru kutoka kwa Mwakilishi wa Benki ya NMB Roman Degeleki katika hafla iliyofanyika katika hospitali ya wilaya mjini Tunduru
Mwakilishi wa NMB Roman Degeleki akimkabidhi Daktari Mfawidhi wa wilaya ya Tunduru Winferd Rwechungura miongoni mwa vifaa vilivyotolewa na Benki ya NMB
baadhi ya vifaa ambavyo vimetolewa na Benki ya NMB kwa hospitali ya wilaya ya Tunduru ambapo mgeni rasmi kwenye makabidhiano ya vifaa hivyo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiroi
Na Albano Midelo,Tunduru
Benki ya NMB imetoa msaada wa vifaa katika Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma ikiwa ni moja ya Lengo la Benki hiyo kurejesha faida kwa jamii na kuifikia jamii katika mahitaji yao muhimu.
Vifaa ambavyo vimekabidhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru ni Mashuka 150, Vitanda 10, Magodoro 10, Viti vyenye Magurudumu (Wheel chair) 04, Vitenga Wodi (screen cutting) 08 ambavyo kwa ujumla vinagharimu Zaidi ya shilingi milioni 10.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivo Kaimu Meneja wa benki ya NMB kanda ya Kusini Ndg. Romani Degeleki amesema Benki hiyo imetoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii asilimia ya faida katika shughuli zinazofanywa na Benki ya NMB.
“Tunafanya biashara na jamii kwa hiyo kwenye faida ambayo tunaitengeneza kila mwaka tunatenga kiasi cha kuweza kurudisha kwa jamii yetu” Alisisitiza.
Akikabidhiwa vifaa hivyo Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro ameishukuru Benki ya NMB kwa kutoa msaada huo wa vifaa katika hospitali ya wilaya ambapo amesema imeunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita.
Mtatiro amewataka watendaji hasa wanaokabidhiwa vifaa hivyo kutambua majukumu yao na kuweza kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu.
Mkuu huyo wa Wilaya ameiomba Benki ya NMB kuendelea kuunga mkono maendeleo ya wilaya ya Tunduru kwa kuzidi kutanua msaada katika sekta nyingine muhimu kama elimu, na kuwataka kusogeza huduma zao za kifedha hasa maeneo ya vijijini.
“Kitendo mlichokifanya sio tu mmereejesha kwa jamii,bali ni shughuli ya kurejesha kwa mwenyezi mungu, Alisema “kitendo hiki ni kikubwa sana katika wilaya yetu kinaenda kuongeza tija katika sekta ya Afya”.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Masanja Kengese ameishukuru Benki ya NMB kwa kuunga mkono Maendeleo ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia ametoa rai kwa taasisi zingine kuiga jitihada hizi za kusaidia jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Hospitali ya wilaya ya Tunduru Daktari Wilfred Rwechungura amesema vifaa hivyo vitasaidia moja kwa moja wananchi wa Wilaya ya Tunduru, na kuomba kuzidi kuweka kipaumbele katika huduma za Afya.
Benki ya NMB imekuwa ni miongoni mwa benki ambayo inasaidia jamii katika Nyanja za Afya, Elimu na Mazingira na kuweza kuwasogezea wananchi huduma karibu Zaidi.