Kamanda a Polisi mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya leo Oktoba 05, 2023 akiwa katika mahafali ya shule ya sekondari ya kutwa ameshangazwa kwa wahitimu hao kumaliza kwa idadi ya wanafunzi 81 tu wakati walipokuwa wameanza kidato cha kwanza walikuwa 202.
Kamanda Mallya akiwa mgeni mualikwa alitumia fursa hiyo kukemea mambo ambayo yanafanya wanafunzi kutokumaliza shule kama wazazi kuwa walevi wa kupindukia, kuamini imani za kishirikina, kuwaruhusu watoto kwenda kufanya kazi za majumbani, kuwaruhusu wanafunzi kwenda kwenye shughuli za uchimbaji wa madini wilayani Chunya, tamaa ya mali ikiwa ni pamoja na kuwafanyia ukatili kama ukatili wa kingono na vipigo.
Aidha, Kamanda Mallya aliwasihi wazazi na wananchi walioudhuria mahafali hayo kuacha mara moja vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto kwani hawataweza kukwepa mkono wa sheria.
Naye Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Dkt. Sister Shitindi kutoka Mkoa wa Kipolisi Kinondoni akiwa kama mgeni rasmi katika mahafali hayo alitoa kiasi cha shilingi Laki 5 kwa ajili ya kununua Printer na vifaa vya michezo ili kuwezesha shughuli za kitaaluma shuleni hapo na kujenga afya ya akili na mwili kupitia michezo kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Sambamba na hayo wazazi, walimu na wanafunzi wamelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa kuendelea kushirikiana na wananchi katika suala la utoaji elimu kuhusu ukatili na usalama wa raia na mali zao.