Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo leo Oktoba 5, 2023 amekabidhiwa Uenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Afrika (AICAD) inayohusika kujengea uwezo Vyuo Vikuu na Jamii katika masuala mbalimbali ikiwemo Kilimo, maji na kuongeza thamani.
Prof. Nombo anapokea nafasi hiyo kutoka Kenya kwa ajili ya kuongoza kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2023.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa Prof. Nombo ameshukuru na kupongeza Uongozi uliopita kwa kazi nzuri, huku akisisitiza nia yake ya kusimamia malengo ya Taasisi hiyo kikamilifu.
‘’Namshukuru Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kutoka Kenya, hakika umeiongoza Taasisi hii vizuri, mmetusaidia kufika hapa tulipo. Pia naipongeza na kuishukuru menejimenti ya Taasisi akiwemo Mtendaji Mkuu Prof. Dominic Byarugaba amefanya kazi nzuri kuibadilisha taasisi.
Prof. Naombo amesema kuwa ni heshima kubwa kwa Nchi na kwake kupata nafasi ya kuiongoza Taasisi hiyo muhimu na ameahidi kuwa atajitahidi kutekeleza majukumu yake ya kuongoza Bodi kusimamia taasisi kufikia malengo.
”Ninatarajia ushirikiano wa kutosha kutoka kwenu, kazi yangu ya kuongoza haita kuwa na ugumu wowote, kwa sababu Bodi ipo na ina uzoefu wa kutosha, hivyo ushiriki wa kila mmoja wetu utasaidia kutekeleza shughuli za Taasisi na hivyo kufikia mafanikio.” alibainisha Prof. Nombo.
Akizungumzia umuhimu wa Taasisi hiyo Prof. Nombo amefafanua kuwa AICAD kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kuanzia mwaka 2012 imefanya makubwa sana, mathalani hapa Tanzania imesaidia kuibuliwa kwa Teknolojia mbalimbali.
‘’Mfano wa teknolojia iliyoibuliwa kupitia ufadhili wa JICA ni namna ya kujenga nyumba kwa gharama nafuu, ukienda Chuo cha SUA na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam utakuta teknolojia hiyo inatumika sana kuhakikisha tunajenga nyumba kwa kutumia gharama nafuu’’. Alinena Prof Nombo.
Akiwasilisha taarifa ya makabidhiano kwa niaba ya Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Dr. David Matene ameishukuru Bodi kwa kumpatia ushirikiano katika kipindi chote alichoongoza, pia ameahidi kuendelea kushirikiana na Mwenyekiti mpya kuendelea kuijenga na kiimarisha taasisi hiyo katika kutekeleza majukumu yake.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya AICAD Prof. Dominic Byarugaba amempongeza Prof. Nombo kupokea mamlaka hayo makubwa na yenye malengo mtambuka kwa nchi zote tatu, huku akimuahidi ushirikiano wa kutosha kuhakikisha wanafikia malengo yaliyokusudiwa.
Wakati huo huo amevitaka Vyuo Vikuu vyote kutoka nchi wanachama kutekeleza majukumu kwa kuzingatia ushindani, ikiwemo kuanza kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kubuni na kutumia teknolojia kikamilifu ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Taasisi ya Afrika AICAD inaundwa na serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kenya pamoja na Jamhuri ya Uganda.