Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe akizungumza na wajasiriamali wakati akizindua mafunzo ya ujasiriamali Wilaya ya Mkalama mkoani hapa Oktoba 3, 2023ambayo yatafanyika katika wilaya zote.
………………………………………………
Na Dotto Mwaibale, Singida
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Singida Aysharose
Mattembe ameunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha
wananchi wanajikomboa kiuchumi kwa kuzindua Mafunzo ya Ujasiriamali Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, mafunzo
yenye kaulimbiu isemayo “SINGIDA YA UJASIRIAMALI NA SAMIA
INAWEZEKANA”
Akizungumza wakati akizindua mfunzo hayo Mattembe
alisema yamelenga kuwawezesha
wajasiriamali kujiamini na kuweza kutoka hatua moja kwenda nyingine kiuchumi.
“Mafunzo haya ambayo yatatolewa na wawezeshaji
wabobezi ni muhimu sana kwa wananchi wetu na wajasiriamali kwani yanakwenda
kuchochea uukuaji wa uchumi wao na kujikwamua kiuchumi,” alisema Mbunge
Mattembe.
Mafunzo hayo ambayo yatafanyika katika wilaya
zote za Mkoa wa Singida yatahusisha usindikaji nafaka, matunda, ufugaji bora wa
kuku, kilimo, pamoja na usimamizi wa fedha yameandaliwa na ofisi ya mbunge na
yanatarajiwa kumalizika November 10,
2023.
Aidha, Mattembe amewaomba wananchi kujitokeza kwa
wingi kupata mafunzo hayo na washiriki wayazingatie kikamilifu na kuwa mabalozi
wazuri kwa wengine ili tija iweze kupatikana maana ni mkombozi kwao na jamii
kwa ujumla.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walimshukuru
Mbunge Mattembe kwa kuwajali wananchi na wajasiriamali kwa kuwapelekea mafunzo
hayo yenye lengo la kuwakomboa kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi.