Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo ameitaka Kamati ya Ushauri wa Kisekta ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika kutumia weledi na uwezo wao katika kuunganisha chuo na soko la ajira.
Prof. Nombo ametoa rai hiyo mara baada ya kuzindua Kamati hiyo ambapo amesema ushirikiano kati ya soko la ajira na chuo utakuwa chachu ya maendeleo ya elimu na kutoa wahitimu watakaokuwa na mchango kwa Taifa.
“Nasisitiza Kamati kutambua malengo na kazi zake ili kubaini, kushauri, kupendekeza mahitaji na mwelekeo wa soko la ajira,”amesema Prof. Nombo
Amesema Kamati hizo pamoja na mambo mengine zitatakiwa kutoa ushauri kuhusu uanzishwaji wa programu mpya za shahada zenye kukidhi soko la ajira, kushauri juu ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na Mafunzo kwa wahadhiri na wakufunzi, shughuli za utafiti na ushauri wa kitaalamu utakaofanywa kwa kushirikiana na sekta binafsi na ya umma.
Katibu Mkuu Nombo amekitaka chuo cha Takwimu na vyuo vingine vilivyopata ufadhili na kuanzisha Kamati hizo kuhakikisha zinakuwa endelevu hata baada ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi (HEET) kukamilika.
Prof. Nombo ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mikakati na mipango ya kuhakikisha elimu ya juu inachangia mabadiliko ya kiuchumi nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Dkt. Katunzi amesema Chuo kina malengo ya kukuza uzalishaji na matumizi ya takwimu bora kwa njia ya mafunzo, utafiti na ushauri elekezi
Akizungumzia namna Chuo hicho kilivyonufaika na Mradi wa HEET Dkt. Katunzi amesema Chuo kimetengewa Sh 6,130,959,495.08
Amesema kuhusu utekelezaji wa Mradi mambo ambayo yameshafanyika ni Chuo kununua gari ili kuwezesha utekelezaji wa kazi za mradi, kugharamia shughuli za ushauri na kufanya tathmini ya athari za mazingira na kijamii kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Taaluma chuoni na kufanya utafiti wa kuanzisha programu mbalimbali Chuo hapo.