……………………………………………………
Na Dotto Mwaibale, Itigi
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru
Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim ameridhishwa na kupitisha miradi yote ya
maendeleo iliyopitiwa na kukaguliwa na Mwenge huo wilayani Itigi mkoani
Singida.
Kaim akizungumza na wananchi wa wilaya
hiyo Septemba 27, 2023 ikiwa ni siku yake ya tano ya mbio za mwenge alisema miradi yote imetekelezwa
vizuri na kuagiza ile yenye mapungufu madogo madogo ifanyiwe marekebisho ndani
ya siku tatu.
Kiongozi huyo wa
mbio za Mwenge, alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan
imekuwa ikileta fedha nyingi kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali hivyo ni jukumu la watendaji kuhakikisha wanaisimamia ili iwe
inajengwa kwa viwango vya ubora ambavyo vinaendana na thamani ya fedha na pia
ni njia ya kumuheshimisha.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Manyoni,
Kemirembe Lwota akitoa taarifa ya miradi iliyotembelewa na
kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru alisema ni saba na kuitaja baadhi kuwa ujenzi wa
Hospitali ya Wilaya wenye thamani ya Sh.Bilioni 1.9, ujenzi wa barabara ya
mijini na vijijini ya mita 700 yenye thamani ya Sh.milioni 499.239, mradi wa
maji uliopo Kijiji cha Njirii wenye thamani ya Sh.Milioni 344.9.
Alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa
Shule mpya ya Msingi Ukombozi wenye thamani ya Sh.Milioni 496.4, Shule ya
Msingi Pentagon wenye thamani ya Sh.Milioni 21.5 mradi wa Vijana (VIKUNDI)
wenye thamani ya Sh.Milioni 3.5 na ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
Alitaja programu zilizotembelewa na
Mwenge huo kuwa ni ya mapambano dhidi ya Malaria ambapo katika kipindi cha
Julai 2022 hadi Juni 2023 jumla ya wagonjwa 23,412 walipimwa malaria ambapo
wanaume walikuwa 6,337 na wanawake 17,075.
Programu nyingine iliyotembelewa
ilikuwa ni ya mapambano dhidi ya Ukimwi
na VVU ambapo wilaya hiyo ina asilimia 4 ya watu waishio na maambukizi ya
virusi vya Ukimwi huku idadi ya wanaotumia dawa za ARV ni 3,633 wanaume wakiwa
1,238 na wanawake 2,390.
Programu nyingine ni mapambano dhidi ya
vitendo vya rushwa na kuanzisha klabu katika shule za sekondari, Utoaji wa
elimu kuhusu masuala ya lishe na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Lwota alisema Mwenge huo umekimbizwa
umbali wa kilometa 77.5.ukifanya shughuli za uwekaji wa jiwe la msingi,
uzinduzi na kutembelea miradi hiyo saba na kuwa kauli mbiu ya mbio hizo za
Mwenge wa Uhuru 2023 ni Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya maji kwa Ustawi
wa Viumbe Hai na Uchumi.
Mbunge wa Manyoni Magharibi Yahaya Masare
alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa
ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo na kuwa
hawana cha kumlipa Zaidi ya kumpa kura nyingi katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika mwaka 2025.
Akitoa salamu Mbunge wa Viti Maalum Mkoa
wa Singida, Aysharose Mattembe naye aliungana na viongozi wenzake akiwepo
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida
kumshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya na kutoa fedha nyingi za
kutekeleza miradi ambapo aliwaomba wananchi ilipo miradi hiyo kutunza
miundombinu yake na aliwaomba kuendelea kumuombea kwa Mungu awe na afya njema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Itigi, Hussein Simba alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapa
ruzuku kutoka katika bajeti ya nchi ya
trioni 7 hadi asilimia 100 ambapo wilaya hiyo inapata Bilioni 8.
Simba alisema mambo hayo zamani yalikuwa
hayafanyiki kwani mradi mmoja tu ulikuwa unatekelezwa kwa robo ya bajeti lakini
leo hii wanapata asilimia 100.
Kesho Septemba 29, 2023 Mwenge wa Uhuru
2023 unamaliza mbio zake mkoani Singida na utakabidhiwa Mkoa wa Dodoma.
Vijana wa Skauti wakimvika Skafu Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 wakati wakimkarisha Wilaya ya Itigi kuanza kukimbiza mwenge huo.