Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amezindua mashindano ya mchezo wa bao kwa klabu za wilaya ya Ilemela kupitia mashindano ya The Angeline Jimbo Cup 2023
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo uliofanyika katika ukumbi wa Mtena B kata ya Buzuruga, Mhe Dkt Angeline Mabula amesema kuwa mashindano ya The Angeline Jimbo Cup yamekuwa yakijumuisha michezo ya mpira peke yake ikiwemo mpira wa miguu, mikono, wavu na pete hivyo kwa msimu huu wa sita wa mashindano hayo ameamua kuhusisha na michezo mingine mipya ambayo imekuwa haipewi kipaumbele sana katika jamii ikiwemo mchezo wa bao na karata
‘.. Lengo letu ni kila mwaka kufanya mashindano ya michezo mbalimbali ili kuibua vipaji na wale watakaotaka kusajili wawapate kwa urahisi sasa miaka yote tulikuwa hatushiriki na hii michezo mingine kama ya bao na karata ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amefafanua kuwa uendeshaji wa mashindano hayo ni utekelezaji wa ahadi yake Kwa wananchi wakati anaomba nafasi ya uwakilishi lakini pia ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama chake CCM
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa chama cha Bao wilaya ya Ilemela Ndugu Said Kihongolo amefafanua kuwa mashindano ya Bao kupitia The Angeline Jimbo Cup 2023 yatahusisha vilabu nane vikiwemo klabu ya Mlezi Pasiansi, Nyambiti, Kasimbu Nyakato, Kirumba, Mecco, Nsumba, Kwa msuka na mkudi na kwamba changamoto kubwa inayokabili chama hicho ni kukosa ufadhili wanaposhiriki mashindano tofauti tofauti ya mchezo huo hivyo kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt Angeline Mabula kwa kuasisi mashindano ya The Angeline Jimbo Cup yatakayohusisha na mchezo wa Bao pamoja na ufadhili wake
Bwana Kihongolo pia amemuahidi ushirikiano Mbunge huyo katika shughuli mbalimbali za kijamii anazozitekeleza na kwamba chama hicho cha Bao na watu wake wanathamini kazi kubwa anayoifanya katika kukuza michezo na wataendelea kumuunga mkono