Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani, ikiwa ni ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi hao
Sehemu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na leo wilayani hapo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji
Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Maiko Mganga akizungumza mbele Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete changamoto zinazokikabali Kitengo hicho katika kutimiza majukumu yake wakati kikao na watmishi wa Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Ramadhan Possi akizungumza na Watumishi wa Halmashauri hiyo kabala ya kumkaribisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete kuzumgmza na watumishi hao, ikiwa ni ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi hao
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Halima Ukash akizungumza kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete kuzungumza na Watumishi hao, ikiwa ni ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi hao
Kaimu wa Idara ya Elimu Msingi, Warda Hussein akizungumza mbele Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete changamoto zinazokikabali Kitengo hicho katika kutimiza majukumu yake wakati kikao na watmishi wa Halmashauri hiyo.
Na. Lusungu Helela–Chalinze
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Watumishi wa Umma kuwa tayari kufanya kazi sehemu yoyote watakayopangiwa kwani Utumishi wa Umma ni utayari wa kukubali kufanya kazi mahali popote.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, ikiwa ni ziara yake ya kimkakati ya kusikiliza na kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili Watumishi hao ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Amesema Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora imekuwa ikipokea maombi kutoka kwa wazazi wakiomba kuwabadilishia watoto wao vituo vya kazi pindi wanapopangiwa mikoa ya pembezoni, wakiomba wapangiwe mijini hususan Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza.
Mhe. Kikwete amewasihi wazazi hao kuwaacha watoto wao wakafanye kazi katika vituo walivyopangiwa kwani katika mikoa hiyo ya pembezoni wanaoishi pia ni Watanzania sawa na wale wanaoishi mijini na kwamba nao pia wanahitaji kuhudumiwa kama wengine.
“Watumishi wenzangu hakuna Watumishi ambao ni maalum kwa ajili ya kufanya kazi mikoa ya pembezoni hivyo nawasihi mtulie kwenye vituo vya kazi mlivyopangiwa na kuendelea kuwahudumia wananchi” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Naibu Waziri Kikwete ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada za kuweka mazingira mazuri ya watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi katika vituo vyao vya kazi.
Katika hatua nyingine Mhe. Kikwete ameahidi kuendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa Halmashauri hiyo huku akiahidi kuzichukua baadhi ya changamoto za kimuundo ambazo zimekuwa zikipunguza morali ya utendaji kazi kwa baadhi ya Wakuu wa vitengo vya Halmashauri hiyo.