Na Mwandishi wetu – Mwanza
Waandishi wa Habari nchini wameaswa kuwawezesha wananchi kutumia takwimu za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 ili kujiletea maendeleo endelevu kwa kutumia takwimu za matokeo hayo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza Mhe. Amina Makilagi leo Septemba 25, 2023 jijini Mwanza wakati alifungua mafunzo kuhusu usambazaji wa matokeo ya Sensa kwa Waandishi wa Habari wa mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza CPA Amos Makala.
“Bajeti yetu ya mwaka huu tumeiandaa kwa kuzingatia matokeo ya Sensa hali ambayo tunaamini kuwa itasaidia katika kuharakisha shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Nyamagana na mkoa wa Mwanza”, amesisitiza Makilagi.
Akieleza zaidi amesema kuwa, dhamira ya Serikali ni kuwezesha mwanachi kutumia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi kuleta maendeleo kwa kasi zaidi.
Matokeo ya Sensa ni msingi wa maendeleo ya taifa kwakuwezesha upangaji wa mipango ya maendeleo, sera na programu zenye kuleta maendeleo kwa haraka na kuzingatia mahitaji ya jamii.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanashirikisha waandishi wa habari takribani 80 kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara.
Aidha, Mhe. Makilagi ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanikisha Sensa yenye viwango vya Kimataifa hali inayochochea maendeleo kwa kasi zaidi.
Aliongeza kuwa vyombo vya habari ni daraja kati ya Serikali na wananchi hivyo vina dhima kubwa katika kuwawezesha wananchi kutumia matokeo ya Sensa katika kujiletea maendeleo yao.
Mada zitakazotolewa katika mafunzo hayo ni pamoja na Majukumu ya NBS, Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 Kidigitali, Wajibu wa Vyombo vya Habari katika Kusambaza Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, Mwongozo wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 na Wajibu wa Vyombo vya Habari katika Kusambaza Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.