Na Mwamvua Mwinyi,Mafia
Wananchi kutoka mikoa ya Pwani na maeneo jirani wanatarajia kushiriki tamasha kubwa la Utalii “Mafia Festival,” litakalofanyika Septemba 28 hadi 30 katika fukwe za Utende zilizopo wilayani Mafia ,mkoa wa Pwani.
Tamasha hilo litahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo kujadili fursa za uchumi wa bluu zinazopatikana kupitia bahari ya Hindi, kilimo cha Mwani , kujionea samaki papapotwe na ufugaji wa Samaki.
Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Zephania Sumaye amesema tamasha litakuwa la kipekee kutokana na eneo hilo kuwa na vivutio vya kitalii vya kipekee.
“Tumejiandaa na amini wananchi watafurahia ,kujifunza na kutalii vivutio vya ndani ya Mafia ,utalii wa boti, jukwaa la biashara litakalojadili fursa za uchumi wa bluu na burudani ,” anasema mkuu huyo wa wilaya.
Akijinasibu na utalii wa papapotwe Zephania alieleza ,kwasasa wamejipanga kuendelea kumtangaza na kutangaza utalii wa Mafia nje na ndani ya nchi ili kupata ongezeko kubwa la watalii.
“Utalii ndani ya kisiwa cha Mafia ni sehemu ya chanzo cha mapato , kutokana na hilo tumaendelea kutangaza kisiwa chetu ,utalii wetu na mengi yanayopatikana ili kujiinua kiuchumi”
Zephania anasema, ili kufikia lengo la makusanyo la halmashauri kupitia utalii ni lazima kujitangaza kiutalii na kubuni vyanzo vipya vya mapato.