Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko akizungumza na wananchi mara baada ya kuwasili katika Jimbo la Bukombe mkoani Geita tarehe 24 Septemba, 2023 kwa ajili ya ziara ya kikazi.
Wananchi wa Jimbo la Bukombe wakimsikiliza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko mara baada ya kuwasili katika Jimbo la Bukombe mkoani Geita tarehe 24 Septemba, 2023 kwa ajili ya ziara ya kikazi.
…….
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo
la Bukombe, Dkt. Doto Biteko ameanza ziara ya kikazi katika jimbo hilo
lililoko mkoani Geita ikiwa ni ziara ya kwanza kufanyika kutoka
ateuliwe na kuapishwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Mara baada ya kuwasili katika Jimbo hilo tarehe 24 Septemba, 2023,
Dkt.Biteko alipokelewa na wananchi wa Jimbo hilo pamoja na viongozi
mbalimbali katika Wilaya Bukombe na Mkoa wa Geita.
Akizugumza katika Mkutano wa hadhara, Dkt.Biteko amemshukuru Rais,
Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kuona kuwa anaweza kumsaidia
katika majukumu aliyokabidhiwa na kuahidi kuwa, atatekeleza majukumu
yake kwa ufanisi katika kuwatumikia wananchi ili kuitendea haki imani
iliyooneshwa kwake.
Amesema kuwa, chini ya uongozi wa Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kila
kitu kilichopangwa kufanyika kinaendelea kufanyika kutokana fedha
anazotoa katika miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo mradi wa umeme wa
Julius Nyerere (MW 2115), ujenzi wa Daraja wa Busisi, ununuzi wa
ndege, madarasa, vituo vya afya, utalii n.k.
Kutokana na hilo, Dkt. Biteko amewataka watendaji na watumishi nchini
kusimamia matumizi sahihi ya fedha za Serikali kwani fedha hizo ndizo
zinategemewa na watanzania katika kuwaletea maendeleo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa Mkoa wa Geita
wamemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini Dkt.Doto
Biteko katika nafasi hiyo kubwa na adhimu na kwamba wana imani kuwa
ataitendea haki nafasi hiyo kutokana na historia yake ya uchapakazi na
uadilifu.
Viongozi hao wakiwemo Wabunge na Wakuu wa Wilaya katika Mkoa wa Geita
wamemshukuru Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi
mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara wilayani Chato, ujenzi wa Chuo
cha VETA wilayani Nyang’hwale na upelekaji umeme vijijini katika
vijiji vya Mkoa huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesifu juhudi
zilizofanywa na Dkt.Biteko wakati akihudumu kama Waziri wa Madini na
kueleleza kuwa amesaidia kuinua mchango sekta ya madini katika uchumi
wa nchi na ameahidi kuwa ataendeleza misingi hiyo mizuri ikiwemo ya
kufanya utafiti wa madini katika eneo lote la nchi ili wachimbaji
wachimbe madini kwa uhakika na hivyo kuongeza mapato ya nchi.
Aidha, ameendelea kusisitiza kuwa, hatalifanyia mzaha suala la
utoroshaji wa madini nchini na kwamba wote watakaotorosha madini
watachukuliwa hatua za kisheria kwani wanakosesha nchi mapato.
kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amemshukuru
Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kugharamia miradi
mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo shule, hospitali
na umeme katika Mkoa Geita.