Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akionesha juu nakala za Mkakati wa Utalii Mkoa wa Ruvuma baada ya kuzinduliwa kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea na kushirikisha wadau kutoka ndani ya Mkoa na wawakishiriki wa Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wengine wa uhifadhi wa kimataifa wakiwemo WWF ,PALM na GIZ
Baadhi ya wadau wa maendeleo na utalii wakiwa kwenye uzinduzi wa Mkakati wa Utalii Mkoa wa Ruvuma
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza kwenye uzinduzi wa Mkakati wa Utalii Mkoa wa Ruvuma
Na Albano Midelo,Songea
Mkoa wa Ruvuma umepokea jumla ya watalii 10,069 ambao wametembelea vivutio mbalimbali katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas wakati anazungumza kwenye uzinduzi wa Mkakati wa Utalii Mkoa wa Ruvuma kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea,
Akizungumza kwenye uzinduzi huo ulioshirikisha wadau kutoka Halmashauri na wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma na wawakilishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,WWF,GIZ na PALM, Kanali Thomas amesema kati ya watalii hao watalii wa ndani walikuwa ni 10,027 na watalii kutoka nje ya nchi ni 69.
“Kwa takwimu hizi kama Mkoa tunahitaji kuongeza juhudi zaidi katika kutangaza vivutio vyetu na kuendelea kuhamaisha zaidi watalii kufika na kutembelea vivutio vyetu’’,alisisitiza Kanali Thomas.
Hata hivyo amesema watalii wengi wanaotoka nje na kutembelea vivutio vya Mkoa wa Ruvuma wanatoka nchi za Zambia,Malawi,Msumbiji,Zimbabwe na Afrika ya Kusini ambapo amesema juhudi ya kutangaza vivutio ikifanyika Mkoa unaweza kupata watalii wengi kutoka nchi za SADC.
Ameyataja malengo ya kuandaa Mkakati wa Utalii katika Mkoa kuwa ni Pamoja na kuitangaza sekta ya utalii,kuongeza uwajibikaji wa kutunza maliasili zilizopo na kuboresha Maisha ya jamii kwa jumla.
Amezitaja nguzo tatu zilizopo katika mkakati huo kuwa ni kuimarisha utendaji kazi wa kitaasisi kwa kushirikiana,kuendeleza utalii unaohusisha utalii wa kihistoria na kiutamaduni na kuwezesha mazingira rafiki ya kuendeleza utalii kwa kuimarisha miundombinu ya usafiri na mawasiliano.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Ruvuma,Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya ameupongeza Mkoa kuzindua mkakati wa Utalii kwa kuwa uhifadhi na utalii ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Mkoa.
Ametoa rai wananchi kushirikishwa kikamilifu kwenye mkakati wa utalii wa Mkoa ili nao wawe sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo kwa kuwa wanahusika moja kwa moja kwenye utalii.
Miongoni mwa vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Ruvuma ni Pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere iliyopo wilayani Namtumbo,Hifadhi ya Taifa ya Mazingira Asilia ya Mwambesi iliyopo wilayani Tunduru,Ziwa Nyasa,Bustani ya wanyamapori ya Ruhila,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Jiwe la Mbuji na Pori la Akiba Liparamba.
Sekta ya Utalii huchangia zaidi ya asilimia 17 katika Pato la Taifa,pia sekta hiyo imeweza kuchangia ajira za moja kwa moja takriban milioni 1.6.