Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi,akizungumza wakati wa Kongamano la siku ya YEMCO VICCOBA 2023 lililofanyoka Jijini Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amezindua Kampuni ya Uwezeshaji na Ubadili wa Ufikiri kwa Vijana (YEMCO MICROFINANCE) itakayohusika na utoaji mikopo kwa vijana.
Tasisi hiyo imezinduliwa Septemba 23, 2023 katika kongamano la siku ya YEMCO VICCOBA 2023 lililofanyoka Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JKICC)
Mhe. Katambi amesema Taasisi ya YEMCO kupitia VICOBA imekuwa mfano wa kuigwa katika kuyawezesha makundi maalumu kuyainua kiuchumi.
Amesema Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwezesha makundi ya Vijana, wanawake na makundi maalumu kwa kutoa mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya Shilingi 1,274,471,500 zimetolewa.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kupitia mafunzo ya Uanagenzi ambapo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016/2017 vijana 78,598 wamenufaika, Vijana 20,334 wamepatiwa mafunzo na kurasimishwa ujuzi walioupata nje ya mfumo rasmi wa mafunzo na kupatiwa vyeti ili wavitumie kutafuta ajira.
Sambamba na hayo, Mhe. Katambi amesema Serikali imeanzisha mafunzo ya kilimo cha kisasa ambapo jumla ya Vijana 13,088 wamepatiwa mafunzo, kati ya hao vijana 12,580 wamepatiwa mafunzo ya kilimo kupitia teknolojia ya kitalu nyumba, vijana 234 mafunzo ya kunenepesha mifugo, vijana 200 mafunzo ya ufugaji samaki na viumbe maji na vijana 74 kilimo cha mazao kupitia vizimba.