Na Mwandishi wetu, Nzega
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdallah Shaib Kaim amezindua mradi wa ‘Bwawa la Kutibu maji taka’ uliotekelezwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Nzega (NZUWASA) kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 1.5.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliopo Nzega Mjini Kiongozi huyo ameupongeza uongozi wa Mamlaka hiyo kwa kusimamia vizuri mradi huo na kuongeza kuwa utasaidia kuboresha usafi na mazingira ya mji huo.
Amesema mradi huo ni muhimu kwani unatekeleza kauli mbiu ya mwenge kwa mwaka huu ambayo inasisitiza juu ya utunzaji mazingira na kuokoa vyanzo vya maji ili kuchochea ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Ameiitaka Mamlaka na wakazi wa Wilaya hiyo kutunza vizuri mradi huo ili udumu kwa muda mrefu na lengo la kuanzishwa kwake lifanikiwe kwa asilimia 100.
Shaib ameiasa jamii kuzingatia elimu ya utunzaji mazingira na kujiepusha na vitendo vyovyote vya uharibifu wa mazingira vikiwemo utupaji taka ovyo, uchomaji taka ngumu holela, ukataji miti ovyo na uharibifu wa miundombinu ya miradi.
Mkurugenzi Mtendaji wa NZUWASA Mhandisi Athuman Kilundumya amemshukuru Rais wa awamu ya sita Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha mradi wa maji wa ziwa Victoria katika Wilaya hiyo na nyinginezo Mkoani hapa.
Amebainisha kuwa baada ya kukamilisha utekelezaji mradi ya maji katika wilaya hiyo Mamlaka iliona umuhimu wa kujenga miundombinu ya kutibu maji taka kwa kuwa asilimia 80 ya maji yanayotumika majumbani hubadilika kuwa majitaka.
Mhandisi Kilundumya amesema mradi huo umehusisha ujenzi wa mabwawa matano yenye uwezo wa kutibu majitaka kiasi cha mita za ujazo 5000 kwa siku na ununuzi wa magari 2 yenye mita za ujazo 10 kila moja.
‘Tunamshukuru sana mama yetu, Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia kiasi cha sh bil 1.586 ili kufanikisha utekelezaji mradi huu wa kimkakati katika mji huu’, amesema.
Ametaja manufaa ya mradi huo kuwa ni kuboresha usafi wa mazingira, kuzuia magonjwa ya mlipuko, kutunza vyanzo vya maji, kutoa ajira kwa vijana na maji taka yanayotibiwa hutumika pia kwa shughuli za kilimo na umwagiliaji.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai amesema mradi huo una manufaa makubwa kwa wananchi wa eneo hilo katika suala zima la utunzaji mazingira.
“Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka huu ikikupendeza tunaomba utuzindulie mradi wetu na pia utuzindulie magari mawili,” amesema DC Tukai.