OR- TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengewa amesema takribani sh. Bilioni 490 zimetumika katika miradi ya maendeleo kwenye halmashauri zote za Mkoa wa Lindi.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo Septemba 19, 2023 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Lindi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya mkoani humo.
Amesema katika Mkoa wa Lindi hakuna Halmashauri, Tarafa, Kata, Kijiji, Kitongoji mpaka mtaa ambao haujapata fedha za miradi ya maendeleo.
Amefafanua mgawanyo wa fedha hizo kwa kila Halmashauri kuwa kwa Manispaa ya Lindi wamepata kiasi cha Sh.Bilioni 105.8, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (sh.Bilioni 148.9) , Mtama (Sh.Bilioni 35), Ruangwa (Sh.Bilioni 77), Nachingwea (Sh.Bilioni 36.6) huku Liwale wakipata sh.Bilioni 85.
“Fedha hizi zote ni za maendeleo na kazi iliyofanyika kwenye eneo la elimu shule zimeongeza na wanafunzi wengi wamepata fursa ya elimu bila malipo, lakini kwenye eneo la afya wananchi sasa wanapata huduma za dharura na huduma za wagonjwa mahututi kwenye EMD na ICU zilizojengwa kwenye maeneo mbalimbali kwenye Halmashauri za Mkoa wa Lindi,”amesema Mhe. Mchengerwa.
Aidha amesema Manispaa ya Lindi itapata Kituo cha Afya kwenye vituo vipya vya afya 214 ambavyo vimeombewa fedha na kabla ya mwaka 2025 kitakuwa kimejengwa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu OR-TAMISEMI kutuma timu kwenye Manispaa ya Lindi kuchunguza mkopo uliokopwa na Halmashauri hiyo bila kufuata taratibu.
Amemshukuru Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha za ujenzi wa miundombinu ya elimu na ambapo leo hii ameweza kufungua shule ya Wasichana ya Sayansi iliyojengwa kupitia Mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambayo kiasi cha sh.Bilioni 4.1 kimetumika kugharamia ujenzi wake.
Mhe. Rais Samia yuko ziarani mkoani Lindi na leo ametembelea na kukagua Miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na Manispaa ya Lindi.