Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (wa pili kushoto) leo Septemba, 2023 akiangalia futi kamba nundu anayoitumia Mwanafunzi asiyeona Magdalena William Buja (wa kwanza kushoto) alipotembelea Chuo cha Ufundi na Marekebisho ya Watu wenye Ulemavu Yombo Dar es Salaam, wa kwanza kulia ni Makamu Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Tungi Mwanjala
Na, Mwandishi wetu.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amejitolea kutimiza ndoto ya Mwanafunzi Magdalena William Buja (23) mwenye ulemavu wa kutoona kwa kumsomesha na kugharamikia matibabu yake ili kutimiza ndoto yake ya kuwa Mwalimu.
Mwanafunzi huyo mwenye ulemavu huo anasoma katika Chuo cha Ufundi na Marekebisho ya Watu wenye Ulemavu Yombo Dar es Salaam ambaye alipata ulemavu huo akiwa kidato cha nne na kushindwa kuendelea na masomo.
Hayo yamejiri Septemba 15, 2023 Mhe. Katambi alipotembelea Chuoni hapo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya Chuo hicho ambapo amesema atahakikisha mwanafunzi huyo anafanyiwa vipimo ili kubaini chanzo cha ulemavu wake.
Amesema majibu ya vipimo yatabainisha kama anaweza kurudi katika hali yake ya awali ama kuendelea na hali hiyo ambapo madaktari watashauri fani anayoweza kusoma ili amsomeshe kuanzia sekondari hadi Chuo Kikuu.
Akitoa neno la shukrani Mwanafunzi huyo, amemshukuru Mhe. Katambi kwa ujio na Uongozi wa Chuo kwa kumfundisha kushona nguo licha ya ulemavu alio nao.