Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha kuanzia Septemba mosi hadi 12, limefanya oparesheni na Misako yenye tija katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mbeya na kupata mafanikio ikiwa ni pamoja na kukamata watuhumiwa 29 wakiwemo wa kupatikana na nyara za serikali (Meno ya Tembo), kufanya uharibifu wa miundombinu ya shirika la umeme (TANESCO) Mbeya na watuhumiwa wanaojihusisha na matukio ya utapeli.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia JOSEPH WILLIAM [30] Mkazi wa Majengo Jijini Mbeya kwa tuhuma za kufanya uharibifu wa miundombinu ya umeme (TANESCO) Mkoa wa Mbeya.
Septemba 05, 2023 huko Mtaa wa Mafiati, Jijini Mbeya, mtuhumiwa alikamatwa akiwa na vifaa mbalimbali vya umeme ambavyo ni Earth Wire, PVC 2.5 meter 7.5, Earth Wire – Bare 3.5 meter 30, Praise moja, Msumemo mmoja ambavyo alikiri kuiba kwenye Transforma ya Umeme Mali ya Shirika la Umeme Tanzania lililopo maeneo ya Hospitali ya K’S.
Aidha, katika upekuzi uliofanywa nyumbani kwake Mtaa wa Nonde Jijini Mbeya alikutwa na vifaa vingine ambavyo ni Solar Street Light Panel yenye 35 watts na Light IP 65 – 200 ambavyo ni mali ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili SYLVESTER RAFAEL @ HAULE [32] Mkazi wa Ipogoro mkoani Iringa na SHUKURU MLOWE [35] Mkazi wa Njombe kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya utapeli kwa njia ya mtandao [simu ya mkononi].
Watuhumiwa walikamatwa Septemba 06, 2023 huko Igawa, Wilaya ya Mbarali na walikuwa wakitafutwa kutokana na kujihusisha na matukio ya utapeli kwa njia ya mtandao was imu katika maeneo ya Jiji la Mbeya, Dodoma, Iringa na Njombe ambapo pia waliruka dhamana ya Polisi.
Watuhumiwa wamekutwa na Gari yenye namba za usajili T.511 DER aina ya Toyota Passo, simu za mkononi 5 ndogo (Analogue) za aina mbalimbali na laini za mitandao mbalimbali.
Aidha, katika muendelezo wa Misako, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari wa TANAPA linamshikilia SELEMAN EZEKIA [34] Mkazi wa Kijiji cha Imalilo Songwe kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali [Meno ya Tembo] mawili yenye uzito wa kilogramu 7.5
Mtuhumiwa alikamatwa Septemba 02, 2023 huko katika Kijiji cha Madundasi Wilaya ya Mbarali katika msako wa Pamoja wa Jeshi la Polisi na Askari wa TANAPA. Mtuhumiwa alikutwa akiwa ameficha nyara hizo kwenye mfuko wa sandarusi ili asafirishe kuupeleka Mbeya Mjini. Taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea.
Vile vile, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Serikali Iyela ya Jijini Mbeya aitwaye YESSE CHARLES [17] kwa tuhuma za kuchoma moto vyumba viwili vya madarasa vya Shule hiyo.
Ni kwamba, Septamba 13, 2023 huko katika Shule ya Sekondari Iyela, Mwanafunzi YESSE CHARLES [17] kidato cha nne alichoma moto vyumba viwili vya madarasa katika Shule hiyo kwa kutumia mabua na karatasi ambapo chumba kimoja kati ya hivyo kilikuwa kikitumika kama bweni kipindi hiki cha likizo kwa baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne walioweka kambi kujisomea kwa ajili ya maandalizi ya mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne.
Chanzo cha tukio ni chuki ya mwanafunzi huyo mtukutu baada ya kuadhibiwa na Mkuu wa Shule hiyo kwa kosa la utovu wa nidhamu na kutokuhudhuria vipindi shuleni hapo.
Moto huo uliteketeza vyumba viwili vya madarasa, nguo, magodoro na madaftari ya wanafunzi. Upelelezi unaendelea.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwimbaji wa nyimbo za injili SIFA BONIVENTURE BUJUNE [25] Mkazi wa Isyesye Jijini Mbeya kwa tuhuma za kuimba wimbo wenye maudhui ya uchochezi na kuurusha kwenye mitandao ya kijamii.
Mtuhumiwa alikamatwa Septemba 13, 2023 huko Isyesye Jijini Mbeya baada ya kuimba wimbo wenye maudhui ya uchochezi dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuusambaza kupitia mitandao ya kijamii pamoja na mtandao wa kurusha maudhui wa Youtube. Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa kwa hatua zaidi za kisheria.
Wakati huo huo, Mnamo tarehe 14.09.2023 majira ya saa 1:30 asubuhi huko katika nyumba za Walimu wa Shule ya Sekondari Mtanila iliyopo Kijiji cha Igangwe Wilaya ya Chunya, Mkuu wa Shule hiyo aliyefahamika kwa jina la MAGWIRA NKUTA [41] alifariki dunia baada ya kunywa kimiminika kinachodhaniwa ni sumu.
Chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo kwani inadaiwa kuwa kabla ya ujio wa mbio za mwenge wa uhuru, marehemu alikabidhiwa fedha na ofisi ya TAKUKURU kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kibao cha “KLABU YA TAKUKURU RAFIKI SHULENI” lakini pamoja na kutumiwa fedha hizo hakuweza kutengeneza kibao hicho hadi Mwenge wa Uhuru ulipofika shuleni hapo kwa ajili ya ufunguzi wa Klabu hiyo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi walioibiwa mali mbalimbali kufika kituo cha Polisi Rujewa, Mbeya Mjini na Chunya kwa ajili ya utambuzi wa mali zao. Aidha, linatoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili wakamatwe na kuchukulia hatua za kisheria.
Imetolewa na:
BENJAMIN KUZAGA – ACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.