Afisa Masoko na Utafiti Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, Sadan Komungoma (katikati) akizungumza na wajasiriamali wakati wa mafunzo ya ufugaji wa mbuzi na kondoo yaliyoandaliwa na VETA kwa wananchi wa Kata ya Unyahati wilayani Ikungi yaliyofanyika Septemba 13, 2023 Chuo cha VETA Ikungi mkoani Singida. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula na kushoto ni Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Ladslous William Mwalimu kutoka VETA Singida.
………………………………………………………………..
Na Dotto
Mwaibale, Ikungi
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi
(VETA) Kanda ya Kati inaendelea kutoa mafunzo ya ufugaji wenye tija wa mbuzi na
kondoo kwa wajasiriamali wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ili waondokane na
ufugaji wa mazoea kwenda kwenye ufugaji wa kibiashara ambao utawakwamua
kiuchumi.
Afisa
Masoko na Utafiti VETA Kanda ya Kati, Sadan Komungoma, akizungumza leo Septemba
13, 2023 wakati wa mafunzo hayo kwa
wajasiriamali wa Kata za Unyahati Kijiji cha Muungano wilayani Ikungi mkoani
Singida alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wananchi kufanya ufugaji
wenye tija na kuwapatia masoko ambayo yatawaongezea kipato.
“Mafunzo haya ni ya awamu ya pili kutolewa
katika Chuo cha VETA Ikungi tangu kilipozinduliwa mwaka jana yanalenga
kuboresha biashara za wananchi ili wafuge mbuzi, kondoo na kuku kwa ubora ambao
utaongeza thamani ya nyama na mayai,” alisema.
Komungoma,alisema VETA imeanza kutoa mafunzo
hayo ya ufugaji wa mbuzi na kondoo kutokana na Mkoa wa Singida kuwa na soko
kubwa la wanyama hao hasa wakati wa Sikukuu ya Eid al-Adha ya kuchinja ambapo maelufu
ya wanyama hao uchinjwa lakini wakinunuliwa kutoka mikoa mingine baada ya Singida
kutokuwa nao wa kutosha.
” Mkoa wa Singida unawaumini wengi wa dini
ya kiislam ambao moja ya nguzo yao kuu ni kutimiza ibada ya chinja ya wanyama
kama ng’ ombe, mbuzi na kondoo ambao kama wangekuwa wanapatikana kwa wingi
wasingekuwa wanakwenda kununuliwa mikoa mingine bali wangepatikana hapahapa na
kuwa fursa kwa wakazi wa Singida,” alisema Komungoma.
Alisema baada ya VETA kufanya utafiti na kubaini
kuwepo kwa soko la wanyama hao ndipo wakaja na mpango wa kutoa mafunzo hayo
yenye lengo la kubadilisha uchumi wa wana Singida kwa kupitia ufugaji wa
wanyama hao ambao hawashambuliwi na magonjwa ya mara kwa mara kama ilivyo kwa
wanyama wengine.
Alisema VETA inatoa mafunzo ya muda mfupi kwa wajasiriamali kwenye mikoa ya kanda ya
kati ambayo ni Dodoma,Singida na Manyara ili kuwawezesha wananchi kunufaika na
uwepo wa vyuo vya VETA vilivyoanzishwa kila wilaya ili wajikwamue kiuchumi
kupitia ujasiriamali na ufugaji.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ikungi, Eva Myula akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo aliwataka washiriki
kuzingatia yale ambayo watafundishwa kwani ni mafunzo yenye tija na yana kwenda
kuinua maisha ya familia na taifa kwa ujumla.
“Hivi sasa ufugaji unafaida sana ukienda
Mnadani kule njia Panda mbuzi mmoja anauzwa hadi Sh.200,000 tofauti na bei
waliyokuwa wakiuzwa zamani nawaombeni zingatieni mafunzo haya kwani ni ya
muhimu sana,” alisema Myula.
Aidha, Myula alisema mafunzo hayo ni fursa kwao
kwani baada ya kuyapata kutapanua wigo wa utafutaji kwa kuuza mifugo yao, mayai
na mazao mengine yanayotokana na wanyama hao na watakuwa wamepata ajira ya
kudumu tofauti na ile ya kuajiriwa kwa mtu au Serikalini.
Myula alitumia nafasi hiyo kuwashukuru VETA kwa
kutoa mafunzo hayo na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fedha kwa ajili ya kuwasaidia watanzania
kukuza uchumi wao.
Washiriki
wamafunzo hayo Mwanahamisi Hamisi, Gangala Nsunaluga, Saida Juma na
Sauli Mayele walisema licha ya kuanza ufugaji tangu siku nyingi lakini walikuwa
hawajui mbinu za ufugaji wa kisasa wenye tija na kuwa wanaishukuru VETA kwa
kuwapa mafunzo hayo.
Mfugaji na mkulima Mariam Ntandu kutoka Kijiji
cha Muungano Kata ya Unyahati, Ikungi anasema anamshukuru sana Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kuwajengea Chuo cha Ufundi cha VETA katika wilaya hiyo na kuwezesha fedha za
mafunzo hayo na kuwa shukurani za pekee ziende kwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA
Kanda ya Kati John Mwanja na watendaji wenzake kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo
yanakwenda kubadilisha maisha yao kupitia fursa za ufugaji wa kisasa.
Alisema shukurani nyingine zimuendee Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi kwa kuwapelekea wataalam
ambao wamekuwa wakiwafundisha mbinu za kilimo na ufugaji bora wa kuku, mbuzi na
kondoo.
Picha ya pamoja