Na. WAF – Songwe
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amebainisha kuwa zaidi ya watoto laki Nne wanatarajia kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio katika Mkoa wa Songwe.
Waziri Ummy ameyasema hayo Septemba 11, 2023 wakati akianza ziara yake ya kukagua huduma zinazotolewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ambapo ameanza kutembelea katika Hospitali ya Wilaya hiyo, Zahanati ya Mbala pamoja na Kituo cha Afya Mbuyuni kilichopo katika Wilaya hiyo.
“Baada ya kupatikana kwa mtoto Mmoja mwenye ugonjwa wa Polio tumeamua kutoa chanjo ya ugonjwa huo ambapo kwa Mkoa wa Songwe tunatarajia kuchanja watoto takribani Laki Nne ambao wana umri chini ya Miaka Nane”. Amesema Waziri Ummy
Amesema, Mwaka 2015 Shirika la Afya Duniani (WHO) iliitangaza Tanzania kuwa ni nchi ambayo imetokomeza ugonjwa Polio, Mwaka huu 2023 Tanzania imepata Mtoto mwenye ugonjwa huo katika Manispaa ya Sumbawanga Mkaoni Rukwa.
“Baada ya Miaka 8 toka WHO iitangaze Tanzania kumalizika kwa ugonjwa wa Polio, Mwaka huu 2023 tumepata mtoto mmoja kutoka Mkoa wa Rukwa ambaye ana virusi vya ugonjwa wa Polio (aina ya Pili)”. Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema kutokana na hatari iliyopo, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI imeamua kuendesha kampeni maalumu ya kutoa chanjo ya kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa Polio.
Amesisitiza kuwa, chanjo hiyo itatolewa katika Mikoa Sita iliyopo mipakani ambayo ni Mkoa wa Songwe, Kigoma, Rukwa, Katavi, Mbeya pamoja na Kagera.
“Mikoa Sita itafikiwa na zoezi hili na lengo ni kuwafikia zaidi ya watoto Mil. 3.5 ambao wana umri chini ya Miaka Nane kwa sababu watoto wote waliozaliwa kuanzia Mwaka 2016 walipata chanjo ya Polio ya kukinga kirusi aina ya kwanza”. Amesema Waziri Ummy
Pia, Waziri Ummy amesema zoezi hilo la utolewaji wa chanjo litaendeshwa kwenye vituo vya kutoa huduma za Afya, mashuleni, nyumba kwa nyumba, sehemu za ibada na vilabuni.
“Wakati wa zoezi hili tutawatumia watu Watatu Watatu katika kila timu ambao watapita kama ni mashambani, mashuleni au masokoni kwa ajili ya kuwapa watoto chanjo hiyo dhidi ya ugonjwa wa Polio ili tuwakinge watoto wetu na ugonjwa huo”. Amesema Waziri Ummy