Mganga Mkuu wa Hospitali ya Jamii Kiuma Mzelifa Masaga akizungumza kuhusu maboresho makubwa ya huduma za matibabu yliyofanyika katika Hospitali hiyo ikiwemo huduma ya kuunga mifupa kwa watu wanaopata ajali.
moja ya vitanda vilivyofungwa kwenye chumba maalum cha upasuaji katika Hospitali ya Jamii Kiuma wilayani Tunduru.
Baadhi ya wataalam wa mionzi wakionyesha vifaa mbalimbali vinavyotumika kwa ajili ya uchunguzi.
Na Muhidin Amri,Tunduru
HOSPITALI ya Jamii Kiuma iliyopo kijiji cha Milonde wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,imekuwa ya kwanza wilayani Tunduru kutoa huduma za kuweka vyuma kwa wagonjwa waliovunjika mifupa baada ya kupata ajali.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt Mzalife Masaga alisema hayo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari waliotembelea Hospitali hiyo ili kujionea kazi ya utoaji huduma kwa wananchi na maboresha mbalimbali yaliyofanyika.
Alisema,wamekuwa wakitumia teknolojia kwenye magonjwa ya mifupa ambayo inasaidia mgonjwa kupona haraka na kuendelea na shughuli zake za uzalishaji mali kwa muda mfupi.
Alisema,Hospitali ya Jamii-Kiuma ilianzishwa mwaka 2004 ili kutoa huduma za afya kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ambao walishindwa kwenda maeneo mengine kupata huduma kutokana na umbali na gharama kubwa.
“kimsingi Hospitali yetu inaendelea kutoa huduma ambazo ni za kijamii kwa gharama ndogo ambazo kila mwananchi anakuwa na uwezo wa kuzifikia ikilinganisha na gharama zinazotolewa na Hospitali nyingine katika ukanda wetu wa kusini”alisema Dkt Masaga.
Alitaja baadhi ya huduma zinazotolewa ni za kimaabara,huduma za mionzi(X-ray)na Utra Sound,huduma za wagonjwa wa nje(OPD)kulaza wagonjwa ambapo jumla ya vitanda 111 vilisajiliwa na huduma za upasuaji ikiwemo tezi dume kwa wanaume wenye umri mkubwa.
Aidha,wanafanya operesheni kwa wanawake wanaoshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida,operesheni za uvimbe na vipimo kwa akina mama wanaoshindwa kushika mimba na huduma zote zenye hadhi ya Hospitali.
Dkt Masaga,ameishukuru Halmashauri ya wilaya Tunduru kuwapatia mtaalam wa meno ambaye amewezesha Hospitali,na wananchi kuanza kupata huduma za meno ambayo haikuwepo tangu Hospitali hiyo ilipoanzishwa.
Askofu wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi Noel Mbawala alisema,kanisa kupitia Hospitali ya jamii- Kiuma limesaidia kusogeza huduma za afya kwa wananchi hasa wanaishi tarafa ya Matemanga na maeneo mengine ya wilaya ya Tunduru.
Kwa mujibu wa Askofu Mbwala,sasa wananchi wa tarafa hiyo hawapati usumbufu wa kwenda hadi Hospitali ya wilaya Tunduru mjini umbali wa kilomita 64 na kilomita 200 kwenda Hospitali ya Rufaa Songea(Homso) kufuata matibabu.
Pia alisema,mama wajawazito wanapata nafasi ya kuhudhuria kliniki baada tu ya kuhisi ujauzito tofauti na hapo awali ambapo baadhi yao walishindwa kuhudhuria kwa wakati kutokana na umbali uliokuwepo.
Aliongeza kuwa,kuanzishwa kwa Hospitali ya Kiuma kwa ujumla imepunguza sana vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua na hata kupungua kwa vifo vya watoto wachanga baada ya kuzaliwa.
Katibu wa Hospitali hiyo Mbarouk Maulid Seleman alisema,katika kutekeleza maagizo na mwogonzo wa serikali wameanza kutoa huduma kwa wagonjwa waliojiunga na Bima ya afya na wametenga wodi maalum kwa ajili yao.
Alisema,hatua hiyo imesaidia sana kuboresha huduma za afya kwa wanachama wakiwemo watumishi wa taasisi ya Kiuma,watumishi wa serikali na wanafunzi ambao ni lazima wawe na Bima ya afya kwa ajili ya matibabu kabla ya kujiunga na shule ya sekondari.
Alisema wodi maalum ya wagonjwa wanaotumia bima, imevutia na kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya baada ya kushuhudia huduma nzuri zinazotolewa ikiwemo kupungua kwa gharama za matibabu ,tofauti na wagonjwa wasiokuwa wanachama ambao wanaolazimika kwenda na fedha nyingi mifukoni ili kugharamia matibabu.
Mkazi wa Milonde Anitha Nchimbi alisema,kuanzishwa kwa wodi ya Bima imekuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wanaofika kupata matibabu katika Hospitali hiyo kwa sababu kwenye wodi mchanganyiko siyo rahisi kupata huduma kwa haraka.
Hata hivyo,ameuomba uongozi wa Hospitali hiyo kuendelea kufanya maboresha ili iwe msaada mkubwa zaidi kwa jamii ya wana Kiuma na wananchi wa maeneo mengine wanaofika ili kupata matibabu.