Na John Walter-Manyara
Serikali imetoa shilingi Milioni 224 kwa ajili ya kukamilisha mradi mkubwa wa maji Dareda-Singu-Sigino,Bagara unaotarajiwa kukamilika septemba 30 mwaka huu.
Jumla ya Gharama za Mradi huo wa Dareda-Singu-Sigino-Bagara wenye kilomita 78 ni shilingi bilioni 12.72.
Katibu Mkuu wizara ya maji Profesa Jamal Katundu akizungumza wakati alipofanya ziara ya kutembelea kujionea hatua za ujenzi huo Dareda na Singu wilayani Babati mkoani Manyara, amewataka wasimamizi Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Mjini Babati (BAWASA) kusimamia kikamilifu mradi ili ukamilike kwa muda uliopangwa.
Hata hivyo Profesa Katundu ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo na kuwapongeza watendaji wa BAWASA huku akiwahakikisha fedha hizo zitafika mapema.
Mradi huo ukikamilika utaufanya mji wa Babati kufikisha asilimia 98 ya upatikanaji wa maji katika mji wa Babati na kuwanufaisha zaidi ya watu 82,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA) Mhandisi Iddy Msuya, amesema pesa walizopewa zitakwenda kuongeza nguvu katika mradi huo na kwamba utakamilika Septemba 30 mwaka huu kama ilivyokusudiwa ili wananchi wafurahie huduma ya maji safi na salama.
Amesema kilio cha wananchi wa Babati kupata maji matamu yasiyokuwa na chumvi kinakwenda kumalizika.